Connect with us

Makala

Wafanyabiashara sita wakiwamo Wachina wafikishwa kortini kwa uhujumu uchumi

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limewafikisha mahakamani wafanyabiashara sita ikiwemo raia wawili wa kigeni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 20, 2019 Kaimu mkurugenzi wa uchunguzi wa Takukuru, Ali Mfuru amesema wafanyabiashara hao wanakabiliwa na mashtaka manane ikiwemo uhujumu uchumi.

Amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakimiliki kampuni maeneo ya Kibaha inayotengeneza na kuuza mafuta aina ya Dizeli yaliyo chini ya kiwango na kuyauzia baadhi ya kampuni zinazofanya biashara hiyo bila kufuata taratibu za ufanyaji biashara.

“Uchunguzi uliofanywa na Takukuru kwa kushirikiana na jeshi la polisi limebaini kampuni ya SHIN UP iliyopo Visiga imejihusisha na vitendo vya rushwa pamoja  na uhujumu uchumi na kusababisha serikali hasara ya zaidi ya 1.2 bilioni,” amesema Mfuru

“Pamoja na mambo mengine, kampuni hii imeghushi vyeti vya kuwawezesha kufanya biashara nchini, inakwepa kodi pamoja na watuhumiwa kujihusisha na mtandao wa uhalifu,” alisema

Amewataja watuhumiwa hao ni Yu Hattao na Zhang Zhi ambao wote ni raia wa China, John Mnyele, Lincolin Ilungu, Andrew Kowelo na Emmanuel Maro ambao ni Watanzania.

Advertisement

Mfuru amesema Oktoba 3O, 2019 Takukuru iliwafikisha mahakamani watuhumiwa watatu kati ya hao ambapo washtakiwa wengine wameeunganishwa nakuongezewa mashtaka yakiwemo utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Mashtaka mengine yanayowakabili ni pamoja na kuendesha biashara ya mafuta bila ya leseni, kujenga kiwanda bila kuwa na kibali na kuendesha kiwanda bila kuwa na cheti cha mazingira.

Mfuru amesema kwa kushirikiana na jeshi la polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini wafanyabiashara wengine walioko kwenye mtandao huo ili kuhakikisha uhalifu huo unatokomezwa.

Comments

More in Makala