Connect with us

Michezo

Tatizo la Samatta ni mafanikio yake mwenyewe


By Ezekiel Kamwaga

KATIKA mchezo wa soka, kuna usemi mmoja mashuhuri kwamba huwa zinatokea siku ambazo mchezaji bora wa mechi anakuwa hayupo hata kiwanjani. Mchezaji bora huyo anaweza kuwa yuko nyumbani kwake anatazama mechi akiwa miguu juu, lakini wanaotazama mechi wote wanaona pengo lake.

Katika miaka ya karibuni, nimewahi kuliona hili miaka takribani miwili iliyopita. Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilikuwa ugenini dhidi ya Lesotho katika michuano ya kuwania kucheza Afcon ya mwaka jana iliyochezwa Misri. Stars ilicheza vema lakini ilifungwa.

Stars ilifanya kila kilichohitajika lakini iliondoka Lesotho patupu. Kwangu, mechi ile ilimkosa mchezaji mmoja tu kutupa matokeo mazuri. Mchezaji huyo si mwingine zaidi ya Mbwana Samatta. Bado naamini kwamba endapo Mbwana angecheza mechi ile, tungeweza kupata walau pointi moja.

Ziko mechi nyingine ambazo pengine hatukustahili kupata chochote lakini kwa sababu ya kuwa na Samatta kwenye timu tulipata walau pointi moja na wakati mwingine zote tatu. Wakati rekodi za Taifa Stars zitakapoanza kuwekwa vizuri, tutakuja kujua kwamba hakuna mchezaji yeyote wa Tanzania ambaye amepachika mabao mengi kumzidi kijana huyu kutoka Mbagala.

Nimefuatilia kwa makini mijadala iliyoendelea baada ya mechi mbili zilizopita za kufuzu kwenye Afcon ya mwaka 2021 nchini Cameroon ambapo Stars imepata ushindi katika mechi moja na kufungwa mechi moja. Mbwana amelaumiwa na baadhi ya washabiki kutokana na namna alivyocheza katika mechi hizo mbili.

Naamini kwamba tatizo kubwa la Samatta ni mafanikio yake aliyoyapata katika mchezo huu na naweza kulieleza hilo katika namna mbili. Kwanza kwa kutumia mfano ambao washabiki wa soka wa Tanzania wanaweza kuuelewa vizuri zaidi na pili mfano ambao unaweza usieleweke vizuri.

Advertisement

Mfano wa kwanza unamhusu mchezaji Simon Msuva. Nimewahi kuwa kiongozi wa Simba wakati Msuva akiwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Yanga. Kwa bahati nzuri mimi ni mpenzi wa masuala ya mbinu na mikakati ya uwanjani na nilikuwa nikisikiliza sana mawaidha ya makocha wa Simba katika mechi zote ambazo ilikuwa inacheza na Yanga.

Karibu makocha wote wa Simba walikuwa wanasisitiza namna ya kuwazuia Haruna Niyonzima na Saimon Msuva wasiwe na madhara.

Ilikuwa inajulikana kwamba endapo timu itaruhusu Msuva na Niyonzima watawale mechi, hali itakuwa mbaya. Matokeo yake yakawa kwamba katika mechi dhidi ya Simba, Msuva akawa hatambi sana. Yakaanza maneno kwamba yeye ni shabiki wa Simba na ndiyo huwa hachezi vema dhidi ya Simba.

Washabiki hawa hawakuwa wakijua kwamba Simba na makocha wake ndiyo wamemfanya Msuva na wakati mwingine Niyonzima washindwe kucheza. ili pia ndilo jambo ambalo limekuwa likimkuta Samatta katika miaka ya karibuni. Mbwana huyu wa leo si yule wa miaka sita hadi minne iliyopita ambaye timu zilikuwa hazimjui.

Leo hii, kila timu inayocheza na Stars inajua ina mchezaji anayeitwa Samatta. Wakati wote wa kujiandaa na mechi zetu, huwa wanakuwa na mikakati ya kuhakikisha nyota wetu huyu anakuwa na athari kidogo kwenye mechi. Kila kocha anakuwa na maelekezo yake kuhusu ni kwa vipi watamdhibiti.

Bado hawajajua sana kumhusu Msuva, Ditram Nchimbi au Iddi Nado. Lakini sasa wanajua kila kitu kuhusu Samatta na ni jambo la akili kwa washabiki na wachambuzi wa soka kufahamu kwamba hiki ni kitu kitakachokuwa endelevu katika miaka inayofuata mpaka nyota huyu wa Genk atakapoamua kutundika daluga zake.

Kwa hiyo hiyo ni sababu ya kwanza na ambayo kwangu ni ya msingi zaidi. Umaarufu wa Samatta utasababisha achungwe zaidi lakini hiyo sasa itatoa fursa kwa akina Msuva kuchomoza. Siku ambayo Msuva naye atakuwa maarufu, tutarajie kumwona akiwa tofauti na alivyo sasa; kama vile Simba na timu za Tanzania zilivyokuwa zikimchunga akiwa Yanga.

Sababu ya pili inahusu sana staili ya uchezaji na tabia ya Samatta. Wengi wa washabiki wa soka bado wanaamini kwamba nahodha ni mtu anayetakiwa kuwa mpambanaji, mlalamishi uwanjani na mtu anayezungumza na kusukuma timu mbele kila wakati. Bahati mbaya ni kwamba Samatta si wa aina hiyo.

Yeye huongoza timu kwa uwezo wake tu uwanjani. Wakati wa mechi dhidi ya Guinea ya Ikweta, Erasto Nyoni alikuwa akizungumza zaidi na waamuzi na kupiga kelele kuliko Samatta ambaye wakati mwingine alikuwa akionekana kujiinamia. Lakini utulivu na ukimya wa Samatta ndiyo imekuwa tabia yake miaka yote tuliyomfahamu. Yeye huacha miguu na kichwa chake vizungumze uwanjani.

Na Samatta, kama walivyo wachezaji wengi wenye vipaji halisi; si aina ya wachezaji wa kukimbizana na kugongana na wenzake uwanjani. Hawa vijana wa Kizaramo na Kindengereko wanaojua mpira wanapenda kucheza mpira tu na si kufanya kazi nyingine za kutumia nguvunguvu.

Hilo wanawaachia akina Elias Maguli, Ditram Nchimbi, Thomas Ulimwengu na wengine ambao Mungu hajawapa kipaji halisi cha kusakata mpira lakini kawapa moyo na mapafu ya kupunguza kile wanachokikosa kwenye uwezo halisi wa kusakata soka.

Kwa hiyo, kumhukumu Samatta kwa sababu hakimbii sana au kupambana huku na kule ni kumwonea. Yeye ana jukumu lake na sehemu kubwa ya jukumu lake liko katika eneo la hatari la wapinzani. Ni sawa na leo mtu aanze kumhukumu Lionel Messi kwamba hakabi anapokuwa uwanjani. Hilo si jambo analoliweza sana uwanjani.

Kwa hiyo tatizo kubwa la Samatta ni mafanikio yake mwenyewe yanayosababisha awekewe mikakati ya kukabwa na timu pinzani na pia kwa washabiki kutegemea makubwa zaidi kutoka kwake kwa sababu sasa wanajua kuwa wana nyota wa kiwango cha juu.

Ni changamoto ambayo Mbwana Ally Samatta anatakiwa kuipokea na kuibeba kwa mikono yake miwili. Wanasema tembo anaponzwa na mkonga wake.


Source link

Comments

More in Michezo