Connect with us

Makala

Serikali ya Tanzania yatakiwa kumlipa fidia mwenye ualbino aliyekatwa mkono

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kamati ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu (CRDP) imeitaka Serikali ya Tanzania kumlipa fidia Mariam Staford, mwenye ualbino aliyevamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana Oktoba 17, 2018.

Mariam (36), alivamiwa akiwa amelala nyumbani kwao kijiji cha Ntobee Wilaya ya Ngara mkoani Kagera na kukatwa mkono mmoja huku mwingine uliokuwa umejeruhiwa kukatwa alipofikishwa hospitali.

Mwaka 2008 watuhumiwa waliohusika na tukio hilo walikamatwa na kufunguliwa mashtaka  katika Mahakama Kuu kanda ya Kagera.

Hata hivyo, waliachiwa huru kwa kile kilichoelezwa kukosekana ushahidi wa kutosha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 21, 2019  mkurugenzi wa shirika la Under the Same Sun, Bethasia Ladislaus amesema kutokana na hatua hiyo, Mariam hakuridhika na uamuzi wa mahakama na kuamua  kutafuta haki katika kamati hiyo.

“Katika kamati hiyo Mariam aliilalamikia Serikali ya Tanzania kutopata haki yake ya msingi kama ibara ya 5,6,8,10,14,15(1),16 na 17 ya mkataba wa kimataifa wa haki za wenye ulemavu ambao Tanzania ni mwanachama tangu mwaka 2009,” amesema.

Advertisement

Amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania ilipata fursa ya kutoa maelezo mbele ya kamati hiyo na kukanusha uwepo wa uvunjifu wa vifungu tajwa na kueleza kuwa ulinzi wa wenye ualbino umeimarisha.

Amesema majibu hayo ya Serikali yalimfanya Mariam kuwasilisha maelezo kinzani dhidi ya Agosti 25, 2016, kutoa utetezi uliokuwa na maelezo tofauti na ya Serikali.

Amebainisha kuwa Januari 16, 2018  Serikali ilikiri kupokea maelezo kinzani ya mlalamikaji, haikuwahi kuwasilisha maelezo mengine ya ziada mbele ya kamati hiyo mpaka hukumu inatoka.

Katika hukumu hiyo, amesema Serikali imetakiwa kumlipa fidia  Mariam,  kumgharamia matibabu yake na kutoa visaidizi (vya mikono)  vitakavyomfanya aweze kuishi kwa kujitegemea.

Akizungumzia suala hilo Mariam amesema amefurahishwa na hukumu hiyo na kubainisha kuwa hana ugomvi na Serikali anachokihitaji ni haki yake.

Amesema kwa hali aliyonayo sasa hawezi kufanya jambo lolote bila msaada wa mtu mwingine.

“Naamini Serikali yangu sikivu itafanyia kazi hukumu hiyo ili na mimi nifanye shughuli zangu maana sipendi kuwa ombaomba barabarani,” amesema Mariam.

Comments

More in Makala