Connect with us

Michezo

Samatta anavyokimbiza rekodi za mabao Ligi ya Mabingwa Ulaya


LONDON, ENGLAND. MATUMAINI ya supastaa wa Tanzania, Mbwana Samatta kucheza kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu yameshindwa kutimia baada ya kikosi chake cha Genk kuwa na hali mbaya huko kwenye Kundi E la michuano hiyo.

Kwenye kundi hilo, Genk inashika nafasi ya mwisho wakiwa wamekusanya pointi moja tu katika mechi tano walizocheza, ambapo wametoka sare moja na vichapo vinne, jambo linalowafanya kuondoka kabla kwenye matumaini ya kutinga hatua inayofuata.

Na sasa mabingwa hao wa Ubelgiji watasubiri tu mchezo wao wa mwisho watakaocheza na Napoli ugenini kwenda kukamilisha ratiba yao na kusubiri msimu ujao.

Lakini, wakati Genk hali yao ikiwa mbaya, michuano ambayo staa wa Tanzania, Samatta alicheza kwa mara ya kwanza haikuwa mibaya kwake kutokana na kile alichokifanya licha ya kwamba hakukuwa na faida kubwa kwa timu yake.

Katika mechi hizo tano, Samatta amecheza kwa dakika 450 na kufunga mabao matatu, huku moja ya bao lake akifunga kwenye uwanja mgumu kwa timu pinzani, Anfield.

Usiku wa juzi Jumatano aliwafunga RB Salzburg kwa mara ya pili msimu huu kwenye michuano hiyo na sasa amebakiza Napoli, ambao atamaliza nao ili kufunga na kuweka rekodi yake tamu ya kuifunga kila timu aliyopangwa nayo kwenye kundi lake.

Advertisement

Si mwanzo mbaya kwa nahodha huyo wa Tanzania kufunga mabao matatu katika msimu wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya huku jambo hilo linamfanya aingie kwenye orodha ya kuwafukuzia mastaa kibao wa Afrika ambao wamefunga mabao mengi kwenye michuano hiyo yenye hadhi kubwa kwa ngazi ya klabu huko Ulaya.

Hii hapa orodha ya wanasoka 10 wa Kiafrika ambao wamefunga mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko Samatta na kufanya afukuzie rekodi zao hizo za mabao.

Yssouf Kone– Burkina Faso, mabao 10

Staa huyo wa zamani wa Burkina Faso, Kone ni mmoja wa wakali wenye rekodi yao tamu ya kufunga mara nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Fowadi huyo aliyekipiga timu kibao ikiwamo Rosenborg, CFR Cluj na Valerenga, ameweka nyavuni mara 10 katika michuano hiyo yenye hadhi kubwa kwa ngazi za klabu huko Ulaya na hivyo kuwa mmoja wa mastaa wa kutoka Afrika walioweka alama zao kwa kufunga mara nyingi kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Dame N’Doye– Senegal, mabao 10

Staa huyo wa Senegal, N’Doye aliwahi kukipiga kwa mkopo Sunderland wakati alipotokea Trabzonspor ya Uturuki. Aliwahi kukipiga pia katika kikosi cha Hull City huko kwenye Ligi Kuu England. Kwa sasa anakipiga FC Copenhagen. Amecheza timu nyingi za Ulaya zilizompa nafasi ya kucheza kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Lokomotiv Moscow na Panathinaikos. Kitendo cha kupewa nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, N’Doye hakufanya makosa, akiweka rekodi ya kufunga mabao 10 na kuwa mmoja wa waliotikisa nyavu mara nyingi.

Obafemi Martins – Nigeria, mabao 10

Straika wa Kinigeria, Obafemi Martins aliwahi kuweka alama zake kwenye Ligi Kuu England wakati alipotua kukipiga kwenye kikosi cha Newcastle United. Na aliwahi kucheza kwa mkopo pia Birmingham City, wakati akitokea Rubin Kazan. Obafemi amevuruga sana kwenye timu za Ulaya, akipita pia kwenye timu za Inter Milan, VfL Wolfsburg na Levante. Kucheza kwenye baadhi ya timu hizo zilimpa Mnigeria huyo nafasi ya kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ambayo alionyesha kiwango chake bora baada ya kufunga mara 10 na kuwa mmoja wa wanasoka wa Kiafrika waliofunga mara nyingi katika mikikimikiki hiyo.

Emmanuel Adebayor– Togo, mabao 14

Straika, Emmanuel Adebayor alitamba sana kwenye Ligi Kuu England alikotua akitokea AS Monaco ya Ufaransa. Kwanza, Adabeyor alisaini kuitumikia Arsenal, ambayo ilimpa nafasi ya kutamba pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. kisha alizichezea pia Manchester City, Tottenham na Crystal Palace huko England, huku akipata pia nafasi ya kukipiga Bernabeu kwenye kikosi cha Real Madrid kwa mkopo.

Kwa sasa staa huyo wa Togo anaichezea Kayserispor ya Uturuki. Muda wake aliocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya haukuwa mbaya, ambapo fowadi huyo alifunga mabao 14 na kuwa mmoja wa mastaa wa Kiafrika waliotikisa nyavu mara nyingi kwenye michuano hiyo.

Pierre-Emerick Aubameyang – Gabon, mabao 15

Supastaa wa Gabon, straika Pierre-Emerick Aubameyang ametua Arsenal kwenye kipindi kibaya wakati timu hiyo ikishindwa kushiriki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, huko Ulaya, Auba amepita kwenye timu nyingi kama Dijon, Lille, Monaco, Saint-Etienne na Borussia Dortmund, ambako alionyesha soka la kiwango cha juu kabisa kuwashawishi Arsenal kutoa pesa ndefu kunasa huduma yake.

Kwa wababe hao wa Ujerumani ndiko Auba alikopata nafasi ya kucheza mechi nyingi za Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumfanya awe amefunga mabao 15 katika michuano hiyo na kuwa staa wa Afrika mwenye mabao mengi katika mikikimikiki hiyo.

Sadio Mane – Senagal, mabao 16

Msenegali, Sadio Mane ni moja ya mastraika matata kabisa kwenye kikosi cha Liverpool kilichobeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita. Kwenye kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp, Mane anaungana na Mohamed Salah na Roberto Firmino kuunda fowadi matata kabisa inayotisha wapinzani.

Mbali na Liverpool, kwenye timu za Ulaya, Mane alizichezea pia Metz, RB Salzburg na Southampton. Ubora wake wa ndani ya uwanja umemfanya kufunga mabao kibao kwenye michuano mbalimbali ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako amefunga mabao 16 na kuweka jina lake kwenye orodha ya wanasoka wa Kiafrika walifunga mara nyingi kwennye michuano hiyo.

Seydou Doumbia – Ivory Coast, mabao 19

Straika wa Ivory Coast, Seydou Doumbia ni moja ya wanasoka wa Kiafrika walioweka alama zao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufunga mara nyingi katika mikikimikiki hiyo. Doumbia alikuwa mtamu zaidi kwenye michuano hiyo katika kipindi chake alichokuwa CSKA Moscow kwa mara ya kwanza kabla ya kurudi tena kwenye timu hiyo kwa mkopo akitokea AS Roma.

Lakini, alichezea timu nyingine kibao kwa mkopo kama Newcastle United, FC Basel na Sporting CP. Kwa sasa anaitumikia FC Sion. Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Doumbia amefunga mabao 19.

Mohamed Salah – Misri, mabao 25

Suala la kufunga mabao halijawahi kuwa gumu kabisa kwa straika wa Liverpool, Mohamed Salah. Jambo hilo limeifanya Liverpool kutamba kwenye michuano mingi ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo walibebeba ubingwa msimu uliopita.

Huko Ulaya, kabla ya kufika Liverpool, Mo Salah amepita kwenye timu za FC Basel, Chelsea, Fiorentina na AS Roma. Huduma yake ndani ya uwanja siku zote ni moto na ndiyo maana amekuwa mmoja wa wanasoka mastaa wa Kiafrika waliofunga mara nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akitikisa nyavu hizo mara 25.

Samuel Eto’o– Cameroon, mabao 33

Kwenye orodha ya mastaa wa Kiafrika wenye rekodi nzuri ya kushinda mara nyingi taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya basi ni Mcamerooni, Samuel Eto’o, ambaye amebeba ubingwa huo mara tatu. Mara mbili alibeba akiwa na Barcelona na nyingine akiwa na Inter Milan.

Eto’o alifunga kwenye fainali zote mbili za kwanza, dhidi ya Arsenal na Manchester United akiwa na Barcelona. Akiwa Inter Milan hakufunga kwenye fainali na kazi hiyo ilifanywa na Diego Milito, aliyefunga mara mbili dhidi ya Bayern Munich. Lakini, rekodi za mabao za Eto’o kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya si haba, akiwa amefunga mabao mara 33.

Didier Drogba– Ivory Coast, mabao 44

Staa wa Ivory Coast, Didier Drogba ndiye baba lao kwa mastaa wa Kiafrika kwa sasa waliofunga mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutikisa nyavu mara 44 kwenye michuano hiyo. Drogba katika msimu wa 2011-12 aliibeba Chelsea kwa mgongo wake kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumfanya aingie kwenye rekodi za kubeba ubingwa wa michuano hiyo.

Kwenye michuano hiyo ya Ulaya, Drogba aliichezea pia Olympique Marseille ya Ufaransa, lakini kubwa ni kuhusu rekodi ya mchezaji huyo kwenye kufunga mara nyingi katika michuano hiyo ya Ulaya na kuwa staa wa Kiafrika aliyewafunika wengine wote kwa kupasia nyavu katika mikikimikiki hiyo yenye hadhi kubwa kwa ngazi ya klabu huko Ulaya.


Source link

Comments

More in Michezo