Connect with us

Michezo

Sadney atoweka , Kalengo afyekwa fasta kisa hiki hapa


By Charity James

MABOSI wa Yanga wameamua kama noma na iwe noma ndani ya klabu hiyo, baada ya kumfuta kazi Kocha Mwinyi Zahera sasa panga linahamia kwa mastaa wao watovu wa nidhamu.

Kwa sasa bundi anaonekana kucheza anga za straika mwenye mwili jumba, David Molinga ambaye taratibu ameanza kuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga pamoja na Sadney Urikhob. Tofauti na Molinga, ambaye kocha wa muda Charles Mkwasa ameahidi kuwa atamchukulia hatua za kinidhamu kwa kuonyesha utovu wa nidhamu wakati akifanyiwa mabadiliko kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania, ambaypo Yanga ilishinda mabao 3-2, Sadney ametoweka kabisa kambini na hajulikani aliko.

Hata hivyo, habari za ndani zinaeleza kuwa Sadney ambaye ameifungia Yanga bao moja kwenye Ligi Kuu Bara akifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Mbao FC, yuko kwenye orodha ya mastaa watakaotemwa dirisha dogo la usajili baadaye mwezi ujao. Imeelezwa kuwa Sadney ametoweka kwa zaidi ya wiki moja huku uongozi hauna taarifa zake na kwamba, taratibu za kuachana naye dirisha dogo zimeanza kutokana na kutoridhishwa na tabia ya utovu wa nidhamu. Mara ya mwisho Sadney raia wa Namibia alionekana kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Coastal Union ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Hata hivyo, chanzo chetu kimeeleza kuwa Sadney amegoma kufanya mazoezi huku sababu za kugomea hazijawekwa wazi.

“Ripoti ya kocha (Mkwasa) ndio inasubiriwa, lakini kwa asilimia kubwa anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wataachwa kwenye dirisha dogo la usajili kutokana na nidhamu pamoja na mchango wake ndani ya timu kutoridhisha,” alisema mmoja wa viongozi ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini. “Kama viongozi lazima tuwe wakali katika hili, timu haijafanya vizuri huku safu ya ushambuliaji ikishindwa kutekeleza majukumu yake uwanjani kisha mchezaji anafanya mambo ya ajabu…hawezi kubaki klabuni.

Wakati Sadney akitoweka, straika Mzambia Maybin Kalengo anasubiri kutangaziwa kutemwa na tayari amerejea nchini kwao.

Advertisement

Kalengo alivunjika mguu kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Pamba uliopigwa jijini Mwanza, ikiwa ni siku chache kabla ya Yanga kuvaana na Pyramids FC kuwania nafasi ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwanaspoti linafahamu kuwa baada ya Kalengo kupata majeraha hayo alisafirishwa kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu, lakini baadaye akaomba kurejea kwao ili kupata matibabu zaidi.

Hata hivyo, habari za kuaminika ndani ya Yanga zinaeleza kuwa straika huyo ambaye hakuonyesha makali yoyote licha ya kutarajiwa kuibeba Yanga, amerejeshwa kwenye klabu yake ya zamani ya Zesco United.

“Kalengo alitua Yanga akitokea Zesco kwa mkopo wa mwaka mmoja na muda aliotakiwa kuwa nje ya uwanja ili kupona majeraha yake utakuwa umemalizika hivyo tumeamua kuvunja mkataba na kumrejesha klabu yake ya zamani,” kilisema.

Kwa sasa Yanga inamfukuzia kwa kasi straika rasta wa Biashara United, Innocent Edwin ambaye anatajwa kuwa mtu sahihi wa kumaliza ukame wa mabao.Mpaka sasa Edwin, raia wa Nigeria ameshaifungia Biashara United mabao matatu na mwenyewe amelieleza Mwanaspoti kwamba hana pingamizi kutua Jangwani kama kila kitu kitakwenda vizuri.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alipoulizwa kuhusu wachezaji hao alikiri Kalengo kwenda kwao, lakini alikanusha taarifa za Sadney kutoweka klabuni hapo , akisema ameshindwa kutumika kikosi cha kwanza cha Mkwasa kutokana na kutokuwa fiti na kwamba, hata mazoezini haonyeshi kupambana ili kumshawishi mwalimu kumpa nafasi. “Mazoezini anakuwepo, lakini haonyeshi kiwango kizuri ambacho kitamshawishi mwalimu ili kumtumia kwenye mechi mbalimbali hasa za Ligi Kuu Bara, tunahitaji matokeo bora kwa sasa ili kupanda nafasi za juu,” alisema Bumbuli.

“Kalengo taarifa nilizonazo ni kuwa amekwenda Zambia kwa mapumziko na kujiuguza jeraha lake, lakini hilo la kuachwa nadhani viongozi ndio wanaweza kulizungumzia.”


Source link

Comments

More in Michezo