Connect with us

Michezo

Mpepo, mtoto wa mtaani anayetaka kuvaa viatu vya Mbwana Samatta


Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ iko vitani katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zitakazochezwa mwakani nchini Cameroon.

Tanzania inawania nafasi hiyo kwa mara ya tatu baada ya kushiriki mwaka 1980 na mwaka huu nchini Misri ingawa mara zote mbili iliaga mashindano hayo katika hatua ya awali.

Taifa Stars iliyopangwa Kundi J ina pointi tatu ilizopata kwa kuifunga Guinea ya Ikweta mabao 2-1 kabla ya kulala 2-1 dhidi ya Libya. Timu nyingine iliyopo katika kundi hilo Tunisia.

Kocha Etienne Ndayiragije ameita jeshi lake kwa mechi hizo na miongoni mwao yumo mshambuliaji anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Buildcon ya Zambia, Eliuter Mpepo.

Mpepo anasema kitendo cha kuitwa Taifa Stars ni bahati kwake kwani amepitia kila aina ya changamoto katika maisha ya kawaida kabla ya kuibukia katika soka.

Akizungumza na Spoti Mikiki, Mpepo anasema hakutarajia kucheza soka kwa kiwango cha ngazi ya klabu ya Ligi Kuu au Taifa Stars kutokana na magumu aliyopitia.

Advertisement

Mchezaji huyo anasema alianza kufanya biashara ya kuchezesha gemu ndani ya vibanda vya mtaani kabla ya soka, kazi ambayo alifanya katika mazingira hatarishi.

“Nimetoka mbali kimaisha nimepata misukosuko mingi hakuna anayeweza kuniamini nilikuwa nikifanya biashara ya kucheza gemu aina ya PES vijana wadogo ambao muda mwingine walikuwa wakitoroka shule,” anasema Mpepo.

Anasema wakati akichezesha gemu, alitenga muda wa kufanya mazoezi na timu za mtaani na baada ya muda aliamua kujikita katika soka na kuachana na biashara hiyo.

Anasema aliyemshawishi kujikita katika soka ni mshambuliaji wa zamani wa Barcelona na nahodha wa zamani wa Cameroon Samuel Eto’o.

Anasema alikuwa akimfuatilia kwa karibu maendeleo ya Eto’o nje ya soka na maisha binafsi, hivyo aliamua kuipa kisogo biashara ya gemu na kuanza kusaka mafanikio ya soka.

Mpepo anasema ndoto ya kucheza soka ilianza kutimia baada ya kujiunga na Prisons ya Mbeya na baadaye Singida United kabla ya kutimkia Buildcon.

“Haikuchukua muda mrefu pamoja na changamoto kadhaa nilipata nafasi Prisons, Singida na sasa nipo Zambia,” anasema Mpepo.

Mshambuliaji huyo anasema Zambia ni moja ya njia yake ya kupata mafanikio katika soka kwa kuwa anaamini ana uwezo wa kucheza nje ya Afrika.

Anasema jezi namba 11 anayovaa imempa changamoto ya kuongeza kasi uwanjani na mkakati wake ni kufikia mafanikio ya wachezaji waliomtangulia akitoa mfano kwa Mbwana Samatta anayecheza Genk ya Ubelgiji na Simon Msuva wa Difaa El Jadida ya Morocco.

“Soka la Zambia ni la ushindani kwa kiwango kikubwa, nadhani kuwa kwao na viwanja vizuri kumechangia ubora walionao kwenye Ligi yao kuhusu jezi niliikuta haina mtu.

“Kama unakumbuka nilifanya vizuri na jezi namba 11 nikiwa Prisons, namba hii haina maana yoyote kwangu lakini ni jezi ambayo ninamapenzi nayo,” anasema.

Wakati maisha ya soka yakiendelea, Mpepo mwenye miaka 19 ana ndoto ya kucheza soka Ulaya.


Source link

Comments

More in Michezo