Connect with us

Makala

Mkwasa apewa kazi kuimaliza Simba SC

By Charity James na Oliver Albert

KAMA kuna shabiki wa Yanga anayefikiria Kocha Charles Mkwasa labda ataondoka hivi karibuni Jangwani baada ya kukaimishwa timu timu kwa wiki mbili mpe pole yake, kwani unaambiwa mabosi wa klabu hiyo wameamua kumuacha hadi pambano la watani wao wa jadi, Simba lipite.

Awali wakati ikitangazwa kutimuliwa kwa Kocha Mwinyi Zahera, Novemba 5 mwaka huu mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla alisisitiza Mkwasa angekaimu nafasi kwa wiki mbili wakati mchakato wa Kocha Mkuu Mpya ukifanyika.

Wiki hizo mbili zilimalizika juzi, lakini jana mabosi wa klabu hiyo walisisitiza Mkwasa hang’oki kwa sasa mpaka kwanza awape kichapo Simba ambao huwa anawajulia kulingana na rekodi walizonazo juu yake.

Dk Msolla jana alitafutwa kufafanua wiki mbili walizotangaza kumkaimisha Mkwasa na mchakato wa kocha mkuu mpya, lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, huku Makamu Mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela akidai alikuwa bize.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema Mkwasa ataendelea kukaimu nafasi hiyo hadi Januari ili kumpa nafasi ya kufanya usajili katika dirisha dogo na kulisimamia pambano la watani wao litakalopigwa Januari 4 mwakani.

“Kwanza Mkwasa ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi, lakini ataendelea kuwa kocha wa Yanga mpaka Januari kwani tunataka kumpa uhuru wa kufanya usajili katika dirisha dogo ili kuiimarisha timu yetu,” alisema Bumbuli na kuongeza;

Advertisement

“Lakini kama itafika Januari na kutakuwa na mchakato wa kupata kocha mpya, Mkwasa anaweza kuomba nafasi hiyo kama atataka, yeye ndiye mwenye maamuzi, ila kwa sasa bado yupo sana Jangwani.”

Hata hivyo, habari za ndani zinadai Mkwasa amepewa muda zaidi wa kuinoa timu hiyo kwa sababu ya mchezo wao dhidi ya Simba utakaofanyika Januari 4.

“Viongozi wameanza harakati za chinichini za kutafuta kocha mpya lakini hawajawaambia ukweli kwani ninavyojua wamemuacha Mkwasa aendelee hadi Januari kwa sababu ya mechi dhidi ya Simba, kwani inaaminika ndiye anayeijua sana Simba na haijawahi kumsumbua tangu akiwa mchezaji na hata kocha na kiongozi wa klabu.

“Ndio maana kakabidhiwa jukumu la kuimaliza siku hiyo,” alisema mmoja kati ya watu walio karibu na uongozi wa juu wa klabu hiyo.

Tangu alipokabidhiwa timu akisaidiana na Said Maulid ‘SMG’, Mkwasa amecheza mechi nne, moja ya mashindano na tatu za kirafiki ambapo ameshinda tatu na kupoteza moja.

Yanga iliifunga Ndanda kwa bao 1-0 katika Ligi Kuu Bara, kisha kuifumua Kombaini ya Nanyumbu kwa mabao 5-0 kabla ya kufungwa 1-0 na Mkuti Market ya Masasi waliocheza nayo mkoani Mtwara kisha kuifunga Coastal Union mabao 3-1 jijini Dar es Salaam zote zikiwa mechi za kirafiki.


Comments

More in Makala