Connect with us

Michezo

Mbivu, mbichi mechi za kufuzu Afcon


By Charles Abel

Dar es Salaam. Raundi mbili za mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Cameroon mwaka 2021, zimekamilika mwanzoni mwa wiki hii.

Zipo nchi ambazo zimejiweka katika nafasi nzuri ya kukata tiketi ya kushiriki Afcon mwaka keshokutwa baada ya kupata ushindi katika mechi zote mbili lakini pia kuna nchi ambazo zimejitengenezea mazingira magumu baada ya kupoteza mechi katika raundi zote mbili kwenye makundi yao.

Kuna mataifa ambayo yamepata matokeo ya wastani yanayozilamisha kukaza buti katika raundi zinazofuata ili kuweka hai matumaini yao ya kwenda Cameroon kulingana na misimamo ya makundi yao yalivyo.

Mashindano hayo yataendelea tena mwakani ambapo raundi ya tatu na nne zitachezwa kati ya Agosti 31 hadi Septemba 8, 2020, raundi ya tano imepangwa kati ya Oktoba 5 hadi 13 mwakani na pazia la mashindano hayo litafungwa rasmi kati ya Novemba 7 hadi 17, 2020.

Kuna mengi yaliyojiri katika mashindano hayo ya kuwania kufuzu Afcon 2021 na Spoti Mikiki linakuletea tathmini ya yaliyojiri katika mechi hizo za raundi ya kwanza na ya pili.

Advertisement

Mataifa manne yaliyowahi kutwaa ubingwa wa Afcon miaka ya nyuma, yameanza vibaya kiasi cha kuweka rehani nafasi zao za kushiriki Fainali hizo mwaka 2021.

Mataifa hayo ni DR Congo, Misri, Zambia na Ivory Coast na sasa yana kibarua kigumu cha kufanya katika raundi nne zilizobaki ili yanusurike.

Mabingwa wa kihistoria wa mashindano hayo, Misri ambao wametwaa taji mara saba (7) wamejikuta wakishika nafasi ya tatu katika kundi G baada ya kutoka sare ya bila kufungana nyumbani na Kenya na mechi iliyofuata wakilazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini na Comoro.

Comoro anaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne, Kenya ipo nafasi ya pili na pointi zake mbili wakati Togo inashika mkia ikiwa na pointi moja.

Kwenye kundi K, Ivory Coast imejikuta ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake tatu ilizopata katika ushindi wa mechi ya kwanza dhidi ya Niger kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Ethiopia na Madagascar inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita huku mkiani wakiwepo Niger.

DR Congo waliotoka sare mbili dhidi ya Gabon na Gambia wanashika nafasi ya tatu kwenye Kundi D wakati Zambia waliotwaa ubingwa wa mashindano hayo mwaka 2012, wanashika mkia kwenye Kundi H baada ya kupoteza mechi zao mbili dhidi ya Algeria na Zimbabwe.

Ushindi katika raundi mbili za mwanzo, umeyaweka mataifa sita katika nafasi nzuri ya kukata tiketi ya kucheza Afcon 2021 huko Cameroon.

timu hizo zinahitaji pointi nne tu katika mechi zao nne zilizobaki ili ziweze kufuzu moja kwa moja mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili.

Mataifa hayo ambayo yanaongoza makundi yao yakiwa na pointi sita ni Ghana iliyo kundi C, Algeria (Kundi H), Senegal (Kundi I), Tunisia (Kundi J), Madagascar (Kundi K) na Nigeria (Kundi L).

Mataifa mawili yanayoonekana vibonde yameleta mshtuko kwa kundi kubwa la mashabiki wa soka baada ya kumaliza raundi mbili yakiwa yanaongoza makundi yao ambayo yanajumuisha timu vigogo.

Ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Angola na sare ya mabao 2-2 dhidi ya DR Congo umeifanya Gambia iliyopo nafasi ya 166 katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kuongoza Kundi D. Ikumbukwe kwamba DR Congo iko katika nafasi ya 54 kwenye viwango vya ubora, Angola iko nafasi ya 120 wakati timu nyingine iliyopo katika kundi hilo, Gabon ipo nafasi ya 87.

Comoro iliyo nafasi ya 142, inaongoza Kundi H ikiwa na pointi nne mbele ya Misri iliyo nafasi ya 49, Kenya (108) na Togo (124)

Madagascar inaendeleza ilipoishia

Moja ya timu zilizokuwa gumzo katika fainali za Afcon mwaka huu ambazo zilifanyika Misri ni Madagascar ambayo licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza, ilionyesha kiwango bora na kuishia hatua ya robo fainali.

Hiyo ni kama imeleta chachu kwa Madagascar kwani wamekuwa moto wa kuotea mbali katika mashindano haya ya kuwania kufuzu fainali za mwaka 2021.

Timu hiyo imekamata usukani wa Kundi K baada ya kuibuka na ushindi katika mechi mbili dhidi ya Ethiopia na Niger. Ilianza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ethiopia na mchezo uliofuata iliangusha kipigo cha mabao 6-2 ugenini ilipocheza na Niger.

Timu hiyo inahitaji pointi nne tu sasa ili itinge Afcon kwa mara ya pili mfululizo.

Ukiondoa Uganda ambayo imekamata usukani wa kundi B ikiwa na pointi nne baada ya kutoka sare na kuibuka na ushindi katika mechi mbili ilizocheza dhidi ya Burkina Faso na Malawi, hali sio nzuri kwa nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki.

Rwanda iliyochezea vipigo katika mechi mbili dhidi ya Msumbiji na Cameroon, inashika mkia wa Kundi F kama ilivyo kwa Burundi ambayo ipo mkiani mwa Kundi E baada ya kufungwa katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Afrika ya Kati na Morocco.

Tanzania ambayo ilianza vyema mashindano hayo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea ya Ikweta, imejikuta ikiangukia nafasi ya tatu katika Kundi J baada ya kuchapwa mabao 2-1 ugenini na Libya juzi, Jumanne iliyopita.


Source link

Comments

More in Michezo