Connect with us

Makala

Mawakala wachangamkie nyota wanawake – Mwanaspoti

MICHUANO ya nne ya Kombe la Chalenji kwa Wanawake kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati, inaendelea jijini Dar es Salaam ikishirikisha timu za nchi nane, wakiwamo wenyeji Kilimanjaro Queens ya Tanzania Bara.

Michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Jumatatu ijayo kwa mchezo wa fainali leo Alhamisi zitashuhudiwa mechi za mwisho za makundi zinachezwa kwa timu za Kundi B, Kenya na Uganda zitakapovaana ili kuamua nani aongoze kundi, huku Ethiopia na Djibouti zikikamilisha tu ratiba.

Watani wa jadi Kenya na Uganda zimefuzu nusu fainali kama ilivyo kwa wenyeji Tanzania na Burundi za Kundi A, watacheza jioni zikiwa zinalingana kila kitu katika kundi lao na mchezo wao ndio utakaoamua nani acheze na Tanzania waliongoza Kundi A na timu ipi icheze na Burundi.

Licha ya kwamba baadhi ya timu shiriki zimekuja kwenye michuano hiyo zikiwa na maandalizi ya zima moto kama ilivyokuwa kwa Zanzibar, Djibouti na hata Sudan Kusini, lakini bado kuna wachezaji wenye umri wenye kutandaza soka kwa uwezo mkubwa. Orodha ya wachezaji walio gumzo kwenye michuano ya safari hii ni wengi, kuonyesha kuwa soka la wanawake linakua kwa kasi.

Baadhi ya nyota walioifanya michuano isisimke na kujadiliwa na mashabiki ni pamoja na Donesia Minja, Opa Clement, Mwahalima Jeriko, Juliet Nalukenge kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Siyo hao kuna wachezaji wengine kutoka Zanzibar, Sudan Kusini, Ethiopia, Burundi na hata Djibouti wameonyesha uwezo mkubwa, kitu ambacho kwa mawakala wa soka hasa kutoka Tanzania tunadhani ni wasaa wao wa kuviangalia vipaji hivyo na kuvitafutia soko nje ya ukanda.

Advertisement

Kwa mfano Tanzania ukiwaondoa kina Donesia na wenzake, hata wale wazoefu na kama kina Mwanahamis Omar ‘Gaucho’, Asha Rashid ‘Mwalala’ na Stumai Abdallah ni wazi kama wangekuwa wana wasimamizi wazuri huenda kwa sasa wasingekuwa wakicheza Tanzania.

Bahati nzuri ni kwamba soka la wanawake kwa sasa limetapakaa karibuni duniani kote, hivyo kama mawakala wataamua kuwasimamia baadhi ya wachezaji wenye uwezo mkubwa wanaweza kuwauza ama kuwatafutia soko nje ya nchi na kusaidia kuitangaza Tanzania kimataifa. Nyota wa timu za wanaume zilizopo nchini ni kama kina Mbwana Samatta, Simon Msuva na wengineo ambao kabla ya hapo walikuwa wakicheza Tanzania kabla ya kuonwa na kuuzwa nje ya nchi. Hatuoni sababu ya kina Mwalala na wenzake ama hao kina Donesia na Opa Clement wamalize soka lao wakiwa Tanzania ilhali wanaweza kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na hata nje ya bara la Afrika kwa vile barani Ulaya kuna klabu kubwa zinamiliki timu za wanawake zinazotetemesha.

Kama miaka ya nyuma Tanzania iliwatoa wachezaji walioenda kucheza Ulaya kama kina Sophia Mwasikili na Esther Chambruma ‘Lunyamila’, kwa nini isiwezekane kwa kina Donesia na wenzake wanaofanya vizuri kwa sasa kwenye soka hilo la wanawake? Hima kwa mawakala, wasiache michuano hiyo imalizike bila kufanya chochote kwa maendeleo ya soka hilo sambamba na kubadilisha maisha ya wachezaji waliojitoa kulinogesha soka la wanawake kwa vipaji walivyojaliwa. Tunaamini kila kitu kinawezekana.


Comments

More in Makala