Connect with us

Michezo

Kilimanjaro Queens shikilieni hapohapo – Mwanaspoti


Mwanzoni mwa wiki hii mechi ya fainali ya michuano ya kuwania Kombe la Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), kwa upande wa wanawake ilipigwa jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 16 hadi 25, ambapo timu ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’ ilicheza na ile ya Kenya ‘Kenya Starlets’.

Katika mchezo huo Kilimanjaro Queens ilipokonywa ubingwa iliokuwa ikiutetea, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Starlets. Queens walikuwa mabingwa watetezi walioshinda ubingwa huo nchini Rwanda mwaka jana.

Mpaka michuano hiyo ilipomalizika katika Uwanja wa Chamazi Complex unaomilikiwa na timu ya soka ya Azam FC, raha ilikuwa ya kipekee kwani mashabiki walijitokeza kwa wingi na kuifanya michuano hiyo kuwa miongoni mwa mashindano yaliyovuta hisia za wengi katika siku za karibuni.

Katika mchezo wa fainali inaelezwa mashabiki wengi walikosa nafasi ya kuingia ndani ya uwanja kutokana na kufurika, na hivyo kulazimika kusikilizia nje kilichokuwa kinaendelea ndani ya uwanja.

Kingine kilichovuta hisia za wengi katika michuano hiyo ni pale kila timu iliyoshinda ilibeba ushindi mkubwa kwani mpizani wake hakujibu hata bao moja na hivyo raha ilikuwa ya aina yake. Mbali na Tanzania Bara nchi zingine zilizoshiriki ni Zanzibar, Kenya, Uganda, Burundi, Djibouti, Ethiopia na Sudan Kusini.

Licha ya kufungwa na kupokonywa ubingwa, Tanzania Bara ndio vinara waliobeba kombe hilo wakiwa wamechukua mara mbili mfululizo mwaka 2016 huko Uganda na 2018 mashindano yalipochezwa Rwanda, huku Kenya ikiwa ni ya pili imefungana na Zanzibar iliyotwaa mwaka 1986 na baada ya hapo yalisimama kwa takribani miaka 30.

Advertisement

Yapo mambo mengi yaliyosisimua katika michuano hiyo mbali na hayo tuliyoyataja hapo juu, lakini kingine ni maandalizi kwa timu kwani zipo zilizojiandaa vizuri na nyingine hazikujiandaa, ndio maana zilizidiana kwa idadi kubwa ya mabao.

Kwa timu zilizofungwa mabao mengi, sababu nyingine inayotajwa kuziathiri ni ile ya hulka ya mwanamke kuwa ni kukata tamaa mapema kwani anapofungwa bao la kwanza anapambana, lakini namna mabao yanavyoongezeka hupoteza nguvu na kupoteana kabisa sababu ikiwa ni kukata tamaa. Mfano mzuri ni katika ile mechi ya fainali na Kenya, baada ya Queens kufungwa ilitoka mchezoni, kwani awali ilijilaumu sana na baadaye ikapotea kabisa kwa sababu ya kufungwa.

Wakati tunawapongeza dada zetu kwa hatua kubwa kufika fainali na hatimaye kuambulia nafasi ya pili, kikubwa ni maandalizi yalitubeba na ndicho kitu muhimu tunachopaswa kutembea kifua mbele tukijivunia kwa timu yetu.

Soka la Tanzania Bara lilivutia na timu ilionekana kucheza kwa mipango, mbinu, ufundi na wachezaji walikuwa fiti kiakili na kimwili wakitumia mfumo wa 3-5-2, huku wakipiga pasi fupi zaidi na ndefu chache na kuwafikia wahusika.

Kutokana na mafanikio hayo hatuna budi kuwapongeza dada zetu kwa kufanikiwa kufikia hatua hiyo, lakini kwa kuendelea kuwa mabingwa wanaoongoza katika ukanda huu. Hata hivyo, kwa upande mwingine mwamko huu wa mashabiki katika kuishangilia timu yetu unapaswa kuendelezwa hata katika michezo mingine kwani huu ndio uzalendo na uanamichezo. Ni vyema tukajipambanua kizalendo michezoni kuonyesha Utanzania wetu.


Source link

Comments

More in Michezo