Connect with us

Michezo

Jinamizi Okwi linamganda beki Alliance FC


By Eliya Solomon

HAKUNA mshambuliaji ambaye alikuwa akimpa wakati mgumu beki wa kulia wa Alliance FC, Israel Patrick kama Mganda Emmanuel Okwi ambaye msimu uliopita alikuwa akiichezea Simba kabla ya kujiunga na Ittehad Alexandria ya Ligi Kuu Misri.

Baada ya kuondoka Okwi, Israel anasema hakuna mshambuliaji ambaye anaweza kumsumbua licha ya uwepo wa Meddie Kagere mwenye mabao saba Ligi Kuu Bara na David Molinga anayetisha huko Yanga.

Patrick ambaye ni mchezaji wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ anasimulia vile shughuli ilivyokuwa katika michezo kadhaa ambayo alikuwa na jukumu la kumzuia Okwi kipindi ambacho mshambuliaji akitesa na Simba.

“Siwezi kusahau ilikuwa mwezi wa 10 mwaka jana, Simba walitufunga mabao matano kwa moja, Okwi aliweza kunisumbua kwa sababu kila nilivyokuwa najipanga kumzuia alikuwa akinizidi ujanja na alinilaza hoi,” anasema.

“Unajua ubaya ni kwamba amekuwa akibadilika na kutumia chenga tofauti, hivyo kama beki sio rahisi kujua namna ya kumzuia, kuna kipindi nilikuwa nikimchezea vibaya nikaona naweza kuigharimu timu.”

Beki huyo aliisaidia Alliance ya Mwanza kuvuna pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Oktoba 23, dhidi ya Ruvu Shooting kwa kufunga bao pekee lililoifanya timu hiyo kufikisha pointi tisa katika michezo sita.

Advertisement

Kupitia kidogo ambacho amekuwa akikipata kwenye soka, Patrick anasema amekuwa akikitumia kwa ajili ya maendeleo ya familia yake huku kingine akikielekeza katika makundi maalumu yenye uhitaji wa misaada.

Patrick anasema huwa hapendi kujigamba na kuzungumzia vile ambavyo soka limemlipa licha ya kuwa bado ana safari ndefu kutokana na umri wake.

“Kuna unafuu wa maisha nauona. Pesa ambayo nimekuwa nikiipata kupitia soka nimekuwa nikiielekeza kwenye familia yangu, ni muda sahihi kwangu, familia yangu kuanza kula matunda ya mchezo ninaocheza hata kama sio kwa kiwango kikubwa,” anasema.

“Kila baada ya muda fulani huwa nimejijengea utaratibu wa kuwatembelea watoto yatima na hata makundi mengine ya uhitaji kwa lengo la kuwafariji, nimetokea katika maisha ya kawaida, napenda kula na wasio nacho.”

Nyota huyo ambaye alianza kusoma shule ya msingi ya Itimbi kabla ya kujiunga na Alliance, anasema hakuwahi kuwaza kufanya kazi nyingine zaidi ya soka na ndio maana ilikuwa rahisi kwake kujiunga na shule ya klabu hiyo, ambayo ilimuendeleza kabla ya kuichezea.

“Tangu nikiwa shule ya msingi nilikuwa nacheza soka, sikuwahi kufanya kazi nyingine na kwa bahati nzuri kipaji changu kilinifanya nichaguliwe kuendelea na Sekondari ya Alliance,” anasema.

Patrick anasema alimudu kucheza madaraja ya chini kabla ya kuipandisha Alliance Ligi Kuu huku akisoma.

“Muda wa kusoma nilikuwa nasoma kweli, sikuwa nataka utani huku nikiweka mkazo na kwenye mazoezi kiasi cha kuingia kwenye timu nikiwa mdogo.”

Tukio la furaha zaidi katika maisha yake ya soka, Patrick anasema ni pale ambapo aliisaidia Alliance kupanda daraja.

Hakuna beki wa kulia ambaye Patrick anamkubali na amekuwa akijifunza mambo mengi kutoka kwake kama Shomary Kapombe wa Simba ambaye pia aliwahi kuichezea Azam FC na kwa Ulaya anasema amekuwa akivutiwa na kiwango cha Kyle Walker anayeichezea Manchester City.

Kuhusu kukutana na ushirikina kwenye uchezaji wake, Patrick anasema pengine ni kutokana na uchanga kwenye soka maana hajawahi kukumbana visa vyovyote zaidi ya kuwasikia wenzake wakisimulia.

“Uchawi upo kwenye soka, lakini sijawahi kukutana nao nadhani ni kwa sababu nimekuwa nikiomba Mungu anisaidie kwenye kila mchezo ili nimalize salama,” anasema.

Patrick ni miongoni mwa makinda wanaochipukia kwa kasi katika Ligi Kuu Tanzania Bara, akitumika mara kwa mara katika ngazi tofauti za taifa huku akiwa na ndoto ya siku moja kuichezea timu ya taifa ya wakubwa ‘Taifa Stars’.


Source link

Comments

More in Michezo