Connect with us

Michezo

Huyo Saliboko humwambii kitu kwa msuli wa Erasto Nyoni


By Charity James

MCHEZO wa soka ni burudani inayoonyeshwa na nyota 11 wanapokuwa uwanjani kwa kucheza na timu pinzani yenye idadi sawa na yao huku wakiwapa burudani watazamaji.

Kwenye soka kila mchezaji anacheza namba ambayo anaamini kwa uwezo wake ndiyo inafaa kupangwa ili aweze kutoa burudani ikiwa ni sambamba na kuipa matokeo timu yake.

Kuna baadhi ya wachezaji wanaweza kucheza namba zote uwanjani. Hao huwa wanaitwa viraka kwa msemo wa mchezo huo, lakini pia kuna wengine wanabadilishwa namba uwanjani kulingana na mwalimu anavyoona kipaji cha mchezaji husika.

Kwenye makala haya Mwanaspoti limepiga stori na msham-buliaji wa Lipuli FC, Daruweshi Saliboko ambaye amefunguka kuwa anafurahia kucheza nafasi ya ushambuliaji kama sehemu aliyocheza tangu akiwa na umri mdogo.

“Unajua mpira ili uufurahie ni kucheza nafasi unayofurahia kucheza, mfano mimi nafurahia kucheza nafasi ninayocheza ambayo inanipa nafasi ya kupambana zaidi ili niweze kuitendea haki kutokana na kuwa na mapenzi nayo,” anasema.

Saliboko anaweka wazi kuwa mchezaji aliyemvutia na kumshawishi kupenda kucheza soka na nafasi ya ushambuliaji ni nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo ‘CR7’.

Advertisement

Pia nyota huyo anaweka wazi kuwa kwa upande wa wachezaji wa ndani, wale wa Kitanzania anamkubali John Bocco anayekipiga kwenye klabu ya Simba.

“Nawashukuru wazazi wangu walikuwa wananipa ushirikiano, hawajawahi kunikatisha tamaa kuhusiana na masuala ya kucheza soka na ndio ninaojivunia hadi hapa nilipofika, na naheshimu ubora wa nyota walionishawishi kupenda soka kutokana na upambanaji wao,” anasema.

Saliboko anasema mbali ya kuwa na mapenzi na nyota hao, pia kwenye uchezaji wake mchezaji ambaye anamsumbua uwanjani pindi anapokutana naye ni Erasto Nyoni anayekipiga Simba FC.

“Nyoni ni beki mzuri ana pumzi, nguvu na ni mtu asiyekubali kushindwa, hivyo unapokutana naye unatakiwa kucheza kwa kutumia akili, na uwe na nguvu nyingi ili uweze kumpita huyo ndio mchezaji tishio kwangu na namkubali kutokana na uchezaji wake.”

Anaweka wazi kuwa mbali na mapenzi yake kwenye soka, pia ndoto yake nyingine nje ya mpira ilikuwa ni kuwa dereva kwani alikuwa anaupenda sana mchezo wa magari na alikuwa anaufuatilia, hicho ndicho kilichokuwa kinamshawishi siku moja na yeye aweze kuwa hivyo.

“Udereva wa magari nilikuwa naupenda sana, lakini nilishindwa kufika huko kutokana na kukosa ushirikiano na kujikuta nafanikisha ndoto yangu moja ya kuwa mchezaji najivunia hilo,” anasema.

USHIRIKINA HAUNA NAFASI KWENYE SOKA

Ushirikina ni jambo ambalo limekuwa likihusishwa kwa kiasi kikubwa katika soka hususani barani Afrika.

Hata katika timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zimekuwa zikifanya baadhi ya vitu ambavyo vinahusishwa na imani za kishirikina.

Saliboko anasema hana imani na imani hizo kwenye uchezaji wake.

“Sijawahi kurogwa wala kuroga na kwa upande wangu siamini kama ushirikina una msaada kwenye mpira,” anasema.

“Ninachoamini mimi ni kwenye upambanaji, kuzingatia mazoezi ili kuwa fiti na sio ndumba.”

Mshambuliaji huyo ambaye amefunguka kuwa akipata ofa ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi yupo tayari kuvunja mkataba na Lipuli.

Mchezaji huyo anacho kikosi chake bora hapa nchini, ambacho kinawahusisha akina Aishi Manura, Shomari Kapombe, Paul Ngalema, Novatus Lufunga, Erasto Nyoni, Mudathir Yahaya, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Meddie Kagere, Daruweshi Saliboko na John Bocco, huku kocha akiwa ni Haruna Heririmana.


Source link

Comments

More in Michezo