Connect with us

Michezo

Genk yatupwa nje Samatta akitupia, Liverpool, Chelsea, Barcelona kama kawa


By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Mshambuliaji Mbwana Samatta amefunga bao lake la tatu katika Ligi ya Mabingwa wakati KRC Genk ikikubalia kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Salzburg.

Samatta alifunga bao lake hilo dakika ya 85 halikutosha kuinusuru KRC Genk kupoteza  katika mchezo huo wa tano katika hatua ya makundi.

Samatta ameendeleza rekodi nzuri dhidi Salzburg kutokana na kuifunga mabao mawili katika michezo miwili waliyokutana, wameendelea kuitesa KRC Genk katika Ligi ya Mabingwa kwa kuvuna pointi zote sita.

Walianza kuzivuna wakiwa kwao Austria ambapo waliifunga KRC Genk mabao 6-2 huku katika mchezo huo wa kwanza kwa Samatta kucheza mashindano hayo, akiweka rekodi ya kucheza kwa mara yake ya kwanza na kufunga bao.

Kipigo cha mabao 3-1 ambacho KRC Genk wenye pointi moja wamekumbana nacho, kinamaana kuwa wametupwa rasmi katika mashindano hayo na hata ile nafasi ya kushiriki Europa Ligi wameipoteza kwani hata kama wataibuka na ushindi katika mchezo wa mwisho hawawezi kumaliza katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Kundi E.

Michezo ya mwisho katika hatua ya makundi, iliyosalia kwa timu za kundi hilo, zitatoa mwelekeo wa timu mbili za kwenda hatua ya mtoano huku moja ikiangukia upande wa Europa Ligi.

Advertisement

Vinara wa kundi hilo ni Liverpool wenye pointi 10, wanafuatiwa na Napoli ambao walitoka nao sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita, Salsburg wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi saba huku Genk wakiburuza mkia na pointi moja.

Ili kusonga mbele kwa Liverpool wanatakiwa kuifunga au kutoka sare dhidi ya Salsburg ambao watakuwa nyumbani, kama watapoteza majogoo hao wa jiji na Napoli akiifunga Genk nchini Italia inamaana kuwa mabingwa hao watetezi wataangukia Europa Ligi.

Wakati hali ikiwa tete kwa KRC Genk katika mashindano hayo, FC Barcelona wamesonga mbele katika hatua ya mtoano baada ya kuifunga Borussia Dortmund mabao 3-1 huku Leo Messi akiweka rekodi ya kufunga dhidi ya timu 34 tofauti katika Ligi ya Mabingwa Ulaya zaidi ya mchezaji yeyote aliyewahi kucheza katika mashindano hayo.

Sare ya mabao 2-2 dhidi ya Benfica, imeifanya Leipzig kusonga mbele katika hatua ya mtoano kutoka kundi G.

Upande wa Kundi H ambalo wapo Chelsea bado hali ni tete, sare ya mabao 2-2 dhidi ya Valencia, imewafanya kuwa katika nafasi ya tatu huku Ajax wakiongoza na Valencia wakishika nafasi ya pili, nafasi pekee kwao ya kusonga mbele ni kuifunga Lille katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi


Source link

Comments

More in Michezo