Connect with us

Michezo

Donisia : Safari ya mkali wa Kilimanjaro Queens


By Doris Maliyaga

UKIMWONA anavyopambana uwanjani hasa kwa wale wanaoamini soka ni wanaume wanaweza kusema hawezi kuwa mwanamke, lakini ukweli bado utabaki pale pale kwa mrembo huyo aliyekamilika.

Hii ni kutokana na ile dhana soka inachezwa na wanaume tu lakini kumbe, wanawake wana uwezo wa kuufanyia maajabu makubwa hadi watu wakashangaa.

Staa huyu wa mashindano ya Cecafa ya Wanawake yanayoshirikisha timu za mataifa manane ya Tanzania Bara, Zanzibar, Burundi, Djibout, Sudan Kusini, Ethiopia, Kenya na Uganda amekuwa moto kama ule wa gesi.

Kiwango kizuri, namna anavyochezesha timu ili ishambulie, kukaba na kupiga mabao, amekuwa kivutio na ukitaka kumjua kodolea mtu anayevaa jezi namba sita mgongoni pindi timu ya Kilimanjaro Queens inaposhuka uwanjani.

Mwenyewe anaweka wazi nguvu alizonazo ni msosi tu wa maana, na chakula anachokipenda zaidi ni wali na maharage, kachumbari, ndizi au tikiti maji na maji ya kunywa ya moto, anamaliza kila kitu.

Pia, mazoezi, nidhamu na ushirikiano pamoja na wenzake ndio umemfikisha hapo alipo na anaweka wazi ndio kwanza anaanza kwa sababu ana mipango mingi siku za mbele.

Advertisement

Shabiki huyo wa Chelsea kwa klabu za nje ya nchi, anasema amezaliwa wa kwanza kwenye familia yake, ana wadogo zake wawili, Peter Minja na David Minja bado wanasoma na wanacheza mpira. Alizaliwa Ukonga, Dar es Salaam Agosti 9, 1999 na sasa ana miaka 20.

“Soka nilianza kujifunza tangu nikiwa mdogo shule ya msingi. Wakati nipo darasa la tatu ndio nilicheza kwa nguvu pamoja na watoto wa kiume,”anasema Donisia mpira huo ulikuwa wa mtaani wanaita Chandimu.

“Sikufundishwa na mtu nilijikuta tu mwenyewe naingia huko ingawa baba na wajomba wangu wanacheza mpira lakini huu wa mchangani.”

Anasema baada ya kumaliza la saba, alijiunga na Simba Queens: “Wakati nacheza Simba Queens ndipo Kipingu aliniona na kunipeleka shuleni kwake nikasoma hadi kidato cha nne. “

“Baada ya kumaliza ndipo nikajiunga na JKT Queens ninayochezea mpaka sasa,”anafafanua Donisia ambaye amepita kwenye timu tofauti za vijana chini ya miaka 17, 20 na sasa mbali na Kilimanjaro Queens ni mchezaji tegemeo wa Twiga Stars.

Kocha Azishi Kondo aliyemwona Donisia anakuwa mpaka sasa anasema, “Kama Donisia ataendelea na bidii hiyo hiyo nidhamu, atafika mbali,”

“Nimemjua tangu alipokuwa mdogo, anakuwa namwona na baba yake, Daniel Minja tunacheza naye mpira mtaani huko kwetu Ukonga kwenye Uwanja wa Gonga na ndio Donisia anaucheza anapokuwa nyumbani.”anasema Azishi.

2018- Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliobeba ubingwa wa Cecafa kule Rwanda

20- Umri wa mchezaji huyo

17 -Umri ambao alianza kuitwa kwenye kikosi cha U17 na baadaye U20

16- Idadi ya mabao aliyofunga msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Wanawake

10- Mabao ambayo ameifungia timu ya taifa kabla ya mashindano ya Cecafa

6- Jezi anayoivaa mchezaji huyo akiwa na Kilimanjaro Queens

5- Idadi ya mabao aliyofunga mpaka sasa kwenye Cecafa

3- akiwa darasa la tatu ndio alianza kujihusisha na soka

2- Idadi ya timu alizochezea Ligi Kuu, Simba Queens na JKT Queens

1- Idadi ya bao alilofunga msumu huu wa Ligi Kuu ya Wanawake

1- Idadi ya Ubingwa wa ligi aliyonyakua.


Source link

Comments

More in Michezo