Connect with us

Michezo

Djibouti: Tumepigwa mabao machache Cecafa


By Doris Maliyaga

TIMU ya soka ya wanawake ya Djibouti ilifungwa jumla ya mabao 33, kwenye michuano ya Cecafa wanawake inayoendelea jijini Dar es Salaam  lakini kocha wa timu hiyo, M’barek Sarah amesema kama wangecheza kwa kutumia falsafa yake, basi wangepigwa mabao mengi zaidi.
Sarah amesema, matokeo ya 13-0 dhidi ya Uganda, 12-0 Kenya na 8-0 Ethiopia si kitu kama wangetumia falsafa yake.
Alisema, mechi moja wangekuwa wanafungwa mabao 30-0 kwenda mbele kwa sababu anapenda soka la kushambulia.
“Katika mashindano haya mbali na kucheza kikubwa tulikuwa tunazuia ili kupunguza idadi ya mabao hatukufunguka kabisa,” alisema Sarah.
“Niligundua kiufundi, fiziki hata mbinu sisi hatuko vizuri na hata tukifunguka vipi ni ngumu kupata matokeo mazuri ndio maana tulizuia zaidi katika mechi zetu zote.”
Alisema, amefurahi kuona timu zimejiandaa na kufanya vizuri katika mashindano haya.
“Nimefurahi kuona timu zinaonyesha ushindani mkubwa jambo ambalo kwa Afrika ilikuwa nyuma, jambo zuri,”alisema.
Kikosi cha Djibouti kilikuwa kimepangwa Kundi B, katika mashindano haya pamoja na Uganda, Kenya na Ethiopia.


Source link

Comments

More in Michezo