Connect with us

Michezo

Dah! Kwa Khamis hakujaeleweka huko Azam


ANAITWA Abalkassim Khamis ambaye amegeuka msugua benchi katika timu ya Azam FC kutokana na kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza.

Khamis yule wa Kagera Sugar ambaye aliisaidia timu hiyo isishuke daraja msimu uliopita na kwa kuifungia mabao sita, sasa amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya muda mrefu, hivyo kushindwa kucheza hata mechi moja tangu Ligi Kuu Bara kuanza.

Kiungo huyo mshambuliaji ambaye alianza kucheza Ligi Kuu Bara 2016 akitokea Zanzibar anasema kuwa soka ndio kazi aliyoichagua, hivyo hakatishwi tamaa na changamoto za kukosa namba kwani anaamini katika upambanaji.

Anasema alianza kucheza Tanzania katika timu ya Tanzania Prisons ambapo alicheza msimu mmoja na baadaye kujiunga na Kagera Sugar ambako alicheza vizuri na kuwavutia viongozi wa Azam FC waliompa mkataba wa mwaka mmoja.

“Kocha ndiye mchezaji namba moja ambaye namhofia kwa sababu ndiye anayenipa nafasi ya kucheza kwa upande wa wachezaji simhofii mtu kabisa,” anasema.

“Najiamini na naamini katika kipaji hakuna mchezaji anayenipa shida, kikubwa ninachokiomba ni Mungu kunipunguzia majeruhi yanayonitesa, hilo ndilo linaninyima namba na sio uwezo,” anasema. Akizungumzia usajili wake wa kwanza akitokea visiwani Zanzibar, akijiunga na Tanzania Prisons , Khamis anasema kuwa ni tukio la furaha kwake na hatalisahau kwani alitoka Zanzibar kucheza Ligi Daraja la Kwanza.

Advertisement

“Tukio langu zuri kwenye soka ni kutoka daraja dogo na kujiunga Ligi Kuu kitu ambacho hakikutegemewa na wengi na hata familia yangu pamoja na kunisapoti kuhusiana na kucheza soka ilijikuta inapata heshima kupitia mimi,” anasema.

USHIRIKINA KWENYE SOKA UPO

Kiungo huyo mshambuliaji anakiri kuwa amewahi kusikia kuwa ushirikina kwenye soka upo, lakini hawezi kuthibitisha kwa sababu haamini kwenye hilo.

“Kuhusu suala la ushirikina unafanyika sana kwenye soka na kuna baadhi ya timu wamekuwa wakiutumia kuhakikisha wanapata matokeo, lakini kwa upande wangu sijawahi kuliamini hilo.”

Alipoulizwa kama amewahi kutumiwa na timu mojawapo kati ya alizochezea kwenda kufanya ushirikina ili waweze kupata matokeo, anakana, huku akisisitiza kuwa kuwa mambo hayo yapo katika mchezo huo unaopendwa na wengi.

CHANGAMOTO ZA SOKA ZINAKUZA VIPAJI

Khamis anasema hakuna kazi isiyokuwa na changamoto huku akiweka wazi kuwa wachezaji wengi wanaopitia changamoto ndio wenye mafanikio.

“Soka ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, hivyo nalo pia lina changamoto zake kama kukosa namba kikosini na majeruhi, ni changamoto ambazo zinakwamisha ndoto za wengi wasiokuwa na moyo wa uvumilivu,” anasema. “Kwa mchezaji anayekubaliana na kila anachokutana nacho kwenye soka huwa anakuwa na ari ya kupambana na mwisho anafanikiwa na kufikia mafanikio.”


Source link

Comments

More in Michezo