Connect with us

Michezo

Azam yachomoa betri kwa Nchimbi


UONGOZI wa Azam FC umeamua kumaliza utata kuhusu mchezaji wao, Ditram Nchimbi anayekipiga kwa mkopo Polisi Tanzania kuwa hakuna ofa yoyote waliyopokea mpaka sasa zaidi ya kusikia maneno tu.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jafar Idi alisema Nchimbi bado ana mkataba wa miezi minane na timu yao na ndio wanaomlipa mshahara, hivyo hawaoni sababu ya kulizungumzia suala ambalo halijawafikia kiofisi.

“Utaratibu wa mpira unajulikana, mtu akimtaka mchezaji lazima awafuate wahusika ndipo waanze makubaliano, sasa wao wanazungumza huko sisi hatuwezi kujibu kitu chochote kwa sababu kinachofanyika ni makosa na ndio maana tumekaa kimya kwani mchezaji huyo yupo Polisi kwa mkopo,” alisema Idi.

Hiyo imetokana na kuwepo kwa taarifa kuwa Nchimbi kaingia kwenye rada za timu kongwe zaSimba na Yanga katika dirisha dogo la usajili huku uongozi wa Polisi ukipambana kumbakiza ndani ya chama lao kwa kumshawishi kumpa ofa ya kazi.

Iko hivi! Wiki iliyopita Mwanaspoti lilimnukuu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Charles Mkumbo akieleza kufurahishwa na uwezo wa wachezaji kadhaa ndani ya timu hiyo akiwemo Nchimbi na kueleza kuwa wamefanya mazungumzo ya kuwapa ajira.

“Nchimbi bado ana mkataba na timu yake, tumefanya naye mazungumzo kutaka kumpa ajira na amekubali,” alisema Mkumbo.

Advertisement

Hata hivyo, Nchimbi alipoulizwa kama yupo tayari kuvishwa gwanda la polisi, alisema: “Hii itanisaidia kimaisha maana nitakuwa nacheza mpira wakati nikiwa na ajira ya kudumu hata kama watu wataongea nini. Inapotokea fursa ya ajira kama hivi inakuwa safi kwani kuna watu wengi wamepitia huko na wamefanikiwa.”

Nchimbi amekuwa akigonga vichwa vya vyombo vya habari baada ya kufunga hat trick kwenye mchezo wa Ligi Kuu katika sare ya mabao 3-3 dhidi ya Yanga, Uwanja wa Uhuru.


Source link

Comments

More in Michezo