Connect with us

Michezo

Aussems awaaga mastaa msimbazi awachomoa Ajibu,Mkude kikosini


HUENDA leo Jumamosi ikawa siku chungu kwa Kocha Patrick Aussems, kielezwa anaweza kukabidhiwa barua yake ya kusitishiwa mkataba Msimbazi, lakini akitambua hana maisha marefu klabu hapo, kiocha huyo kutoka Ubelgiji ameanza kuwaaga rasmi wachezaji wake.

Simba leo Jumamosi itakuwa na kibarua mbele ya Ruvu Shooting katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, lakini unaelezwa utakuwa mchezo wa mwisho wa Aussems kama kocha mkuu wa klabu hiyo.

Inaelezwa Aussems anayetajwa yupo mbioni kutua Polokwane FC ya Afrika Kusini juzi Alhamisi alishindwa kukutana na mabosi wake kwenye kikao, ingawa mapema asubuhi alishiriki mazoezi ya timu kwenye Uwanja wa Uhuru na kueleza kuomba kikao hicho kifanyike jana Ijumaa.

Hata hivyo, mabosi wa Simba wameamua kumkaushia wakitaka amalizane na Ruvu Shooting leo Jumamosi kisha kumalizana naye, na jana kocha huyo aliamua kuwaaga mapema wachezaji wake kuonyesha kwamba anajua kila kitu kinachoendelea dhidi yake.

Ipo hivi. Simba kwa kawaida tangu ikiwa chini ya Aussems kila inapokaribia mechi siku moja huingia kambini wachezaji 18 tu ambao hutumika kwenye mchezo husika, lakini kocha huyo jana aliamuru wachezaji wote kasoro Erasto Nyoni aliye majeruhi wawpo. Lakini kabla ya kuagiza wachezaji wote kwenda kambini, Mbweni pembezoni ya jijini la Dar es Salaam, kocha huyo alizungumza nao mara baada ya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Gymkhana na kuwaaga kimtindo.

Mmoja wa wachezaji wa Simba aliyeomba kuhifadhiwa jina, alisema katika mazungumzo na Kocha Aussems sambamba na wasaidizi wake, aliwaambia kwamba chochote kinaweza kutokea kutokana na taarifa zilizozagaa dhidi yake.

Advertisement

“Alituambia tuachane na taarifa za yeye kufukuzwa kwenye timu na kututaka tuelekeze nguvu zaidi kwenye mechi yetu na Ruvu, ingawa alisema lolote linaweza kutokea kwake na isitushughulishe sana na tufikirie zaidi mechi ya kesho (leo),” alisema mmoja ya nyota hao wa Simba na kuongeza:

“Ndio maana ametaka tuingie kambini wote na kama kutatokea mabadiliko kuhusu suala lake apate muda wa kuongea nasi kwa mara ya mwisho, ila ni mtu ambaye anaonekana ameshaelewa kilicho mbele yake.”

Aussems alipoulizwa juu ya taarifa za kumalizana na Polokwane FC ya Afrika Kusini alisema anashangaa kwanini watu wanataka kufahamu mambo yake binafsi wakati bado ni muajiriwa wa Simba, ndio maana anaendelea na majukumu yake Msimbazi.

“Sioni kama ni jambo rasmi la kueleza hapa kuwa kuna taarifa ya kwenda kusaini timu nyingine wakati bado nipo na mkataba na Simba, ninaoutumikia, narudia nilikuwa na matatizo binafsi na ndiyo yaliyonifanya niondoke ghafla,” alisema Aussems.

“Nina utulivu wa hali ya juu katika timu kwa sasa bila ya kuwaza jambo lolote kwani nguvu na akili yangu tumeiweka katika mechi ya kesho (leo) jioni ili kuweza kupata ushindi, hilo ndilo ninaloweza kusema hizo taarifa nyingine siwezi kulizungumzia.”

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu Kocha Aussems alienda Afrika Kusini na kuanzia juzi taarifa zimeanza kuvuja taarifa kwamba anajiandaa kuwa kocha wa Polokwane FC iliyopo Ligi Kuu ya nchini humo maarufu kama PSL.


Source link

Comments

More in Michezo