Connect with us

Michezo

Aussems asimamishwa kazi Simba Sc


By KHATIMU NAHEKA NA OLIPA ASSA

Dar es Salaam.Simba imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi kuu Bara baada ua kuenguliwa kwa saa 24 na Kagera Sugar baada ya kuifumua Ruvu Shooting kwa mabao 3-0, lakini mara baada ya ushindi huo mabosi wa klabu wakamsimamisha rasmi Kocha Mkuu wao, Patrick Aussems kwa saa 120.
Habari kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo na zilizothibitishwa na Aussems mwenyewe ni kwamba kocha huyo kushindwa kuitikia wito wa kikao alichokuwa akutane na Afisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa sambamba na vigogo wa Simba na kuwakera mabosi hao.
Alhamisi ikiwa ni siku moja tangu Aussems arejee nchini kutoka kwenye safari yake binafsi alikuwa akutane na Senzo pamoja na Kaimu Rais wa klabu hiyo Mwina Kaduguda kwa mazungumzo juu ya kuondoka kwake ghafla nchini akitoa taarifa akiwa Uwanja wa Ndege akijiandaa kuanza safari.
Kukwama kwa kikao hicho kuliwatibua zaidi mabosi wa klabu hiyo huku mjadala tangu jana ukiwa ni kumzuia kocha huyo kukaa benchi kwenye mchezo wao na Ruvu uliopigwa Uwanja wa Uhuru.
Hata hivyo baadaye mabosi hao walifuta uamuzi huo, huku wakibaki na kosa moja la kumtaka kumjadili kocha huyo kwa kosa la kuondoka kwake nchini.
Hata hivyo Mwanaspoti limejulishwa kuwa Simba unatafuta usahihi wa kocha huyo kutimkia Afrika Kusini ikielezwa tayari yuko katika hatua za mwisho endapo itathibitika alikwenda kufanya mazungumzo na moja ya klabu za nchini humo.
“Unajua kama tukipata uhakika wa kama amefanya mazungumzo na klabu ya Afrika Kusini, yeye na klabu hiyo itajuta kuijua Simba, hii sio Simba ya kuchezewa tutatoa fundisho kwao,” alisema mmoja wa wajumbe wa bodi.
Mwanaspoti linafahamu Senzo ndiye anayefanya vurugu za kutafuta ukweli wa taarifa hizo za Aussems, ingawa amekuwa akikutana na ugumu wa kupata uhakika wa 100 % ingawa klabu ya Polokwane imemfuta kazi kocha wake aliyekuwa anaiongoza timu hiyo.

APEWA BARUA
Jana baada ya Simba kumaliza mchezo wa Ruvu, ambapo mshambuliaji Miraj Athuman alifunga mabao mawili, moja kila kipindi na lingine la beki Mbrazili, Tairone Da Silva na kuwarejesha kileleni walipoondolewa na Kagera Sugar juzi Ijumaa ilipoifunga Lipuli mabao 2-1, Aussems alikutana na mabosi wa klabu hiyo kisha akakabidhiwa barua ya kusimamishwa hadi kikao cha Bodi kitakakutana na kutoa maamuzi ya mwisho Alhamisi ijayo. Muda huo wa kusimamishwa kwake ni kama siku tano tangua kuanzia leo Jumapili ambazo ni sawa na saa 120.
“Tumeamua kumsimamisha kwanza unajua bodi inaona kama ametufanyia (Aussems) dharau zilizopitiliza tutamjadili na kutoa uamuzi baadaye wiki ijayo.”

AUSSEMS AKIRI KILA KITU
Kufuatia taarifa hiyo Mwanaspoti lilimtafuta Aussems, aliyethibitisha kupokea barua hiyo.
Aussems alisema kwa sasa anawasiliana na wanasheria wake kutoka Ulaya kumpa ushauri wa hatua za kusimamishwa kwake.
Mazungumzo na Aussems na Mwanaspoti yalikuwa kama ifuatavyo;
Mwanaspoti: Patrick habari?
Aussems: Salama rafiki habari ya kwako?
Mwanaspoti: Huku salama hongera kwa ushindi mzuri.
Aussems: Ahsante sana ni ushindi muhimu hasa unapotokea katika mapumziko ya mechi za Kimataifa na ukizingatia tulipata sare mchezo uliopita nyumbani.
Mwanaspoti: Wakati timu ikipata ushindi huu tumepata taarifa kwamba umepata barua ya kusimamishwa kina ukweli gani katika hili au nalo bado ni uvumi?
Aussems: Nikweli nimepokea hiyo barua ya kunipa hayo maamuzi.
Mwanaspoti: Pole sana Patrick sasa klabu imesema sababu ni ipi?
Aussems: Wanasema ni juu ya kutokuwepo kwangu nchini kwa siku mbili nafikiri ni wakati nilipokwenda kitatua mambo yangu binafsi.
Mwanaspoti: Kwa hiyo umesimamishwa kwa muda gani au barua inasemaje muda wa kusimamishwa kwako?
Aussems: Ni mpaka kikao cha bodi kitakachokaa Novemba 28, ndio watatatoa maamuzi hivyo nasubiri.
Mwanaspoti: Patrick wewe kama muajiriwa wa Simba umeamua kufanya nini baada ya uamuzi huo wa klabu?
Aussems: Unajua haya maamuzi nimeyapokea muda mchache baada ya mechi kumalizika sasa nimeanza kuwasiliana na Wanasheria wangu Ulaya kujua kipi nifanye. Unajua uamuzi huu unafanya niwe nje ya majukumu yangu ni muhimu kuwashirikisha watu wa sheria kwa upande wangu pia.
Mwanaspoti: Sawa Patrick nafikiri acha tusubiri kuona Simba itaamua nini.
Aussems: Ahsante rafiki karibu sana.
Mwanaspoti: Ahsante sana na usiku mwema.
Aussems: Na kwako  pia.


Source link

Comments

More in Michezo