Connect with us

Michezo

Arsenal sasa yamtaka yule kocha wa Wolves


LONDON, ENGLAND . UPEPO unabadilika kwa kasi pale Arsenal na maisha yanaenda haraka zaidi. Habari ya mjini ni uvumi unaoendelea kuhusu kufukuzwa kwa kocha wao, Unai Emery. Lakini kizaazaa kipo kwa nani anaweza kuchukua kiti chake.

Baada ya uvumi wa Arsenal kuonyesha kwamba klabu hiyo ilikuwa inajiandaa kumchukua kocha wa zamani wa Tottenham, Mauricio Pochettino kibao sasa kimegeuka na habari zinadai kwamba kocha wa Wolves, Nuno Espirito Santo sasa anaongoza katika mbio za kuchukua kiti hicho.

Unai amekalia kuti kavu zaidi baada ya Arsenal kutoa sare ya tatu mfululizo katika Ligi Kuu ya England baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbanbi dhidi ya Southampton wikiendi iliyopita na inadaiwa kwamba mabosi wa Arsenal sasa wanasaka mtu wa kuchukua nafasi yake.

Awali mabosi wa Arsenal walitoa kauli kwamba bado wapo nyuma ya kocha huyo raia wa Hispania, lakini baada ya sare dhidi ya Southampton huku Arsenal wakiendelea kucheza mpira usioeleweka kiasi cha timu kuzomewa na mashabiki mara baada ya mechi hiyo, mabosi wanaonekana kubadilisha msimamo.

Santo ameibuka kuongoza katika mbio hizo akipewa alama 9/4 na hii inatokana na urafiki mkubwa uliopo kati ya mkuu wa kitengo cha michezo wa Arsenal, Raul Sanllehi na wakala wa Santo, Jorge Mendes ambaye ni miongoni mwa mawakala maarufu wa soka duniani.

Santo amewakosha mabosi wa Arsenal kutokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa na Wolves ambapo kocha huyo Mreno mwenye umri wa miaka 45 aliiongoza Wolves kupanda Ligi Kuu misimu miwili iliyopita na msimu uliopita aliipeleka katika michuano ya Europa kwa kushika nafasi ya saba.

Advertisement

Msimu huu Wolves walionekana kushindwa presha ya kumudu kucheza michuano ya Europa na ligi kwa pamoja, na walianza ligi ovyo, lakini sasa Santo ameirudisha timu hiyo katika mstari na sasa inashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu huku katika michuano ya Europa wakiwa katika nafasi nzuri ya kutinga makundi.

Arsenal wanaweza kwanza kumuondoa Emery na kuicha timu katika mikono ya wasaidizi, Fredrick Ljungberg ambaye ni staa wa zamani wa timu hiyo pamoja na kocha wa timu ya vijana, Steve Bold ambaye pia ni staa wa zamani wa Arsenal.

Makocha wanaopewa nafasi achilia mbali ni pamoja na staa wa zamani wa timu hiyo, Mikel Arteta anayepewa alama 3/1, kocha wa zamani wa Juventus Maxi Allegri anayepewa alama 5/1, Rafa Benitez anayepewa alama 6/1, kocha wa Bournemouth, Eddie Howe alama 8/1 na Pochettino anayepewa pia alama 8/1.

Emery anatazamiwa kukalia benchi katika pambano la leo la michuano ya Europa dhidi ya Eintracht Frankfurt ya Ujerumani lakini kuna uwezekano mkubwa akaondolewa katika nafasi yake kama Arsenal itafungwa au kutoka sare dhidi ya Norwich City.

Arsenal imeanza kuwa na wasiwasi kwamba huenda ikawapoteza mastaa wake wawili Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette kama timu hiyo itaendelea kulegalega chini ya Emery na kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa mara nyingine.

Aubameyang ambaye alikuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya England msimu uliopita sambamba na mastaa wa Liverpool, Sadio Mane na Mohamed Salah – wote wakiwa na mabao 22 ameanza kunyatiwa kwa kasi na klabu mbili kubwa za Hispania, Real Madrid na Barcelona. Taarifa kutoka katika gazeti la The Mirror la Uingereza zinadai kwamba Lacazette alibwatukiana na kocha huyo wakati pambano dhidi ya Southampton likiendelea licha ya kuifungia Arsenal mabao yote mawili ambayo yaliiokoa na kipigo.


Source link

Comments

More in Michezo