Simba: Ligi inachelewa

0
48
  • ***Leo inacheza na Namungo FC huku ikifungua Uwanja wa Majaliwa ulioko Lindi…

WAKATI mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatarajia kuwakabili Namungo FC katika mechi ya kirafiki itakayofanyika leo kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Lindi, benchi la ufundi la timu hiyo limesema kuwa wanaona muda wa kuanza kipenga cha msimu mpya wa 2018/19 unachelewa.

Mabingwa hao wa Bara watafungua pazia la ligi kwa kuikaribisha Tanzania Prisons Agosti 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati Yanga wenyewe siku itakayofuata watakuwa ugenini kucheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema kuwa kikosi cha timu yao kiko tayari kuanza msimu mpya na wanaamini wataendelea na kasi waliyokuwa nayo katika msimu uliopita.

Djuma alisema kila mchezaji wa Simba ana “uchu” wa kuonyesha ufundi wake na hii inatokana na kupata muda mzuri wa kufanya maandalizi kuelekea kutetea taji wanalolishikilia.

Alisema kuwa wamejiandaa kukabiliana na ushindani na changamoto za ndani na nje ya uwanja kutoka kwa timu zote, kwa sababu wanafahamu ligi hiyo ya juu Tanzania Bara haitakuwa nyepesi.

“Tuko tayari kuanza msimu mpya, tunajua haitakuwa kazi nyepesi, kila mechi kwetu itakuwa muhimu, tunajua msimu huu ushindani utakuwa umeongezeka na hatutadharau timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu,” alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa Simba ina kikosi “kipana” na hivyo msimu huu kila mchezaji atapata nafasi ya kuisaidia timu kupata matokeo mazuri kwenye mechi za nyumbani na ugenini.

Wakati huo huo kikosi cha Simba kilifika salama Lindi tayari kwa mchezo huo wa kirafiki unaofanyika sambamba na ufunguzi wa uwanja mpya wa Majaliwa ambao umejengwa na Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa.

Baada ya mechi hiyo, Simba itaelekea jijini Arusha kucheza mechi nyingine ya kirafiki halafu itaelekea Mwanza kuvaana na Mtibwa Sugar katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani itakayofanyika Agosti 18 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here