Mapya yaibuka kuhusu King Majuto

0
21

Mapya yaibuka kuhusu King Majuto

ZIKIWA zimepita siku mbili tangu msanii  maarufu a vichekesho nchini, Amri Athumani, maarufu kama ‘King Majuto’ azikwe shambani kwake Kiruku, Tanga,  mambo mapya yameibuka.

Imebainika kwamba msanii huyo ambaye alikonga nyoyo za Watanzania kwa muda wote wa uhai wake,  alikuwa na malengo makubwa ya kuwasaidia Watanzania wenzake mambo makubwa ingawa amekufa kabla ya kutimiza ndoto zake.

King Majuto alikuwa na ndoto ya kununua gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwasaidia majirani zake wanapopata dharura hasa nyakati za usiku.

Majuto pia alikuwa na ndoto ya kujenga hospitali shambani kwake ambayo ingewahudumia wananchi bila malipo kuanzia tiba na dawa.

Kwenye mahojiano yake na Channel ya Danga Chee, Majuto alisema anataka akumbukwe kwa kufanya vitu vikubwa kwenye jamii badala ya kukumbukwa kama mchekeshaji.

Alisema anataka kununua gari la kubeba wagonjwa baada ya kushuhudia wagonjwa wakibebwa kwenye baiskeli wanapougua hasa nyakati za usiku.

“Vijijini watu wanaenda mbali kutibiwa wagonjwa wanapanda baiskeli. Unakuta  baiskeli imefungwa miti halafu amelazwa mama mjamzito na barabara mbaya mwisho wa siku anampoteza mtoto,” alisema.

Kuhusu hospitali, alisema anatarajia kuijenga na kwamba  ingekuwa na chumba cha daktari, sindano, kufunga vidonda na chumba cha kupumzika wagonjwa waliozidiwa.

“Itakapokamilika nitaiomba serikali inipatie bure madaktari na manesi. Nitawalipa  ila kama serikali ikitaka kunisaidia kuwalipa nitashukuru,” alisema.

“Nataka watu wazungumzie King Majuto aliacha nini siyo alikuwa anachekesha kama Mr. Bean (mchekeshaji maarufu raia wa Uingereza). Yote haya nayafanya kijijini kwangu Kiruku, Tanga, watibiwe bure na kusoma bure na watakunywa chai na kwenda nyumbani,” alisema.

Majuto alisema atakaponunua gari la wagonjwa atakuwa anafanya kazi ya kuwasafirisha watu wa jirani yake bila kuwatoza chochote hata ikiwa usiku wa manane.

Alisema amejenga msikiti shambani kwake ambao watu wanautumia kuswali pamoja na  madrasa kwa ajili ya kuendelea elimu ya dini.

“Sihitaji msaada ni kwa pesa zangu nahangaika ili waje waongelee vizuri Majuto kaacha nini siyo vichekesho pekee au kalifanyia nini taifa,” alisema.

MGANGA WA TIBA ZA ASILI

Majuto alisema alikuwa anatoa huduma ya uganga wa tiba za asili kwa wananchi ingawa wakati akiwa kwenye shughuli za uigizaji, alikuwa akimwachia mtu aiendeleze.

“Nikiwa kwenye majukumu yangu ya uigizaji kuna mtu ninamwachia anawatibu wananchi na mimi nikipata muda nakwenda kuendelea kutoa tiba,” alisema.

Alipoulizwa suala la kugombea nafasi yoyote ya uongozi, Majuto alisema hapendi kuwa kiongozi.

“Sitaki kuwa kiongozi kwa sababu hiyo itanibana katika shughuli zangu za kuigiza. Utajikuta unaamua masuala ya watu, kuzungumza na watu au kuzungumzia shughuli za nchi. Hadi umri huu  sijaupata uongozi, siutaki,” alisema.

Akizungumzia familia yake na kama kuna waliorithi kipaji chake, Majuto alisema watoto wake wamemrithi isipokuwa mmoja ambaye anajishughulisha na muziki wa dansi.

Katika mahojiano hayo, Majuto alisema atastaafu uigizaji pale ambako atashindwa kuongea.

Aidha, alisema uigizaji umemwezesha kujenga nyumba mbili, mabanda ya kufugia kuku na shamba kubwa ambalo amepanda matunda ya aina tofauti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here