Unashangaa ya Karius? Yaone ya CR7, Messi

0
7
KURUDIWA kwa wimbo wa ‘You’ll Never Walk Alone’, lazima kuonekane hakukuwa na maana yoyote kwa Loris Karius Jumamosi usiku wa Mei 26, mwaka huu, baada ya kufanya makosa mawili makubwa yaliyoigharimu Liverpool kushindwa kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Kunesa kwa mashabiki wa Liverpool kulielekea moja kwa moja kwa kipa huyo raia wa Ujerumani aliyeomba radhi kwa kuigharimu timu.
Lakini Karius siyo mchezaji wa kwanza kusababisha kilio hicho kwa timu yake, sasa ni kazi kwa kipa huyo  kuungana na wenzake hawa ili kuhakikisha haonyeshi tena kiwango kibovu. Hawa ni wachezaji sita ambao walisababisha balaa kama la Karius…
6. Cristiano Ronaldo (vs Austria, 2016)
Katika mechi ya pili ya Ureno kwenye michuano ya Euro 2016, Cristiano Ronaldo alikuwa na wakati mbaya kwenye mechi hii. Alibeba jukumu la kupiga penalti waliyozawadiwa dakika za mwisho, lakini alishindwa kuizamisha kimyani.
Lakini Ronaldo alirejea mchezoni kwenye mechi iliyofuata dhidi ya Hungary, akifunga  mabao mawili na kuiwezesha Ureno kutinga hatua ya 16-Bora. Pia alifunga dhidi ya Wales katika hatua ya nusu fainali ingawa majeraha yalimfanya kuikosa mechi ya fainali dhidi ya Ufaransa, Ureno ilitwaa ubingwa kwa kushinda 1-0.
5. Patrice Evra (vs Man City, 2006)
Natumai alikuwa katika kiwango cha juu wakati Manchester United ilipomsajili beki huyu wa kushoto, Patrice Evra, kutoka Monaco mwaka 2006, lakini pengine mechi ya ‘dabi’ dhidi ya Manchester City haikuwa wazo la njia sahihi kwake kuweza kuzoea. Evra hakuweza kwenda sambamba na kasi ya Premier League na alitolewa wakati wa mapumziko huku akitupiwa jicho baya.
United hatimaye, ilipoteza kwa mabao 3-1, lakini uwapo wa Evra United ulikuwa wa mafanikio zaidi kwa miaka ya baadaye. Aliibuka kuwa mchezaji muhimu United akitwaa mataji mawili; la Premier League na la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008, huku akishinda jumla ya mataji matano ya ligi katika kipindi chake cha miaka tisa Old Trafford kabla ya kuondoka mwaka 2014. 
4. Zlatan Ibrahimovic (vs Cesena, 2010)
Zlatan Ibrahimovic amekuwa na mafanikio katika kila klabu aliyoichezea hadi alipokumbwa na msuguano wakati akiitumikia Barcelona. Alijaribu kurekebisha kazi yake kwa kujiunga kwa mkopo AC Milan, lakini alianza kwa staili isiyosahaulika kufuatia ‘Rossoneri’ hao kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Cesena, huku Ibrahimovic akikosa penalti dakika za mwisho.
Lakini huwezi kumweka ‘mbwa’ mzuri nyuma, kwani mabao 22 aliyofunga katika mashindano yote huku wakitwaa ubingwa wa Serie A, Milan iliridhia kumpeleka Ibrahimovic San Siro jumla. Mabao mengine 35 yalikuja mwaka uliofuata ambayo yalikuwa ni idadi bora zaidi katika wasifu wake, jambo lililoishawishi PSG kumfuata na kumsajili majira ya joto ya msimu huo. 
3. Jamie Carragher (vs Man Utd, 1999)
Lilikuwa ni jambo jema kuona Jamie Carragher akimfariji Karius baada ya mechi hiyo ya Jumamosi Mei 26, mwaka huu. Nguli huyo wa Liverpool anajua ni kwa namna gani unajisikia baada ya kufanya makosa katika mechi, alijifunga mabao mawili katika mechi moja mwaka 1999. Na kufanya tukio hilo kuwa baya, wapinzani wa Liverpool siku hiyo walikuwa ni Manchester United, ambao walishinda 3-2, shukukrani kwa ukarimu wa Carragher.
Carragher ndiyo kwanza alikuwa na miaka 21na kipindi cha miaka mitatu kuitumikia Liverpool wakati huo. Lakini miaka iliyofuatia, Carragher alipata mafanikio na aliifungia jumla ya mabao nane kwa kipindi chake chote akiwa Anfield.
2. Lionel Messi (vs Hungary, 2005)
Kwa mchezaji ambaye kamwe hajawahi kuwa na wakati mbaya kimchezo, ni kitu kigeni kudhani kukumbwa na kipindi kibaya zaidi kwake kuwahi kutokea – na kwa kifupi ilikuwa ni kwenye mechi yake ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Hungary mwaka 2005. Aliingia dakika ya 63 akitokea benchi, lakini alitolewa baada ya dakika tatu akituhumiwa kumpiga kiwiko Vilmos Vanczak.
Je, alihitaji hata kusema nini kilichotokea tena? Messi ameibuka kuwa kinara wa ufungaji wa wakati wote Argentina, akiwa na mabao 64 na katika macho ya wengi, mchezaji mkubwa zaidi duniani.
Kama Argentina itatwaa Kombe la Dunia majira haya ya joto na Messi kustaafu baada ya hapo, Tofauti kati ya mechi yake ya kwanza na ya mwisho itazungumzwa sana kwa mtu huyu ambaye anafanya soka kuangaliwa kama mashairi. 
1. Ronaldo (vs Ufaransa, 1998)
Inachukuliwa kama stori kubwa zaidi katika  ukombozi wa soka lake, lakini Ronaldo hawezi kulaumu kwa kiwango alichoonyesha mwaka 1998 katika fainali ya Kombe la Dunia. Alikumbwa na mshtuko saa chache kabla ya mechi na kisha kwenda kupumzika kabla ya kumshawishi kocha Mario Zagallo kumjumuisha katika kikosi. Uamuzi huo uliwagharimu, alicheza kwa taabu, na kisha Brazil kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Ufaransa.
Kuanzia hapo, Kombe la Dunia 2002, Ronaldo alionekana kama mtu wa kazi. Alitwaa Kiatu cha Dhahabu, akifunga jumla ya mabao nane kwenye michuano hiyo, lakini kwa kuifunga tu Ujerumani katika mechi ya fainali kilikuwa kipindi kizuri cha ukombozi kwake. Ronaldo aliifungia Brazil mabao yote wakati ikishinda 2-0, lakini mwaka 1998 hausahauliki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here