Manji arudisha shangwe Yanga

0
9
KAMA hauamini basi shauri yako, Yanga walikuwa wanalia ukata na sasa tajiri wao namba moja, Yusuf Manji, yupo mlangoni na mpaka sasa ni uhakika atatua pale Bwalo la Polisi kwenye Mkutano Mkuu wa klabu hiyo kesho Jumapili.
Wanachama na mashabiki wa Yanga wanakubali klabu yao kuingia katika mchakato wa mabadiliko ya uwekezaji, lakini jina wanalotaka lifanye uwekezaji huo ni Yusuf Manji.
Yanga inafanya mkutano mkuu kesho, lakini Mwanaspoti linafahamu mbali ya kuwaalika baadhi ya viongozi wa Serikali na TFF wakiongozwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, lakini mtu mwingine atakayetingisha mkutano huo ni Manji.
Mabadiliko yakoje
Yanga inataka kufanya mabadiliko katika mfumo wake wa uendeshaji, lakini tayari wanachama kupitia viongozi wa matawi wameshafanya vikao kutaka mchakato huo ufanyike kwa haraka na umhusishe Manji.
Mmoja wa viongozi wa matawi Edwin Kaisi, amesema wamekubali mabadiliko na katiba yao inayatambua ila Manji ashirikishwe kwani tayari alishafanya makubwa ndani ya klabu hiyo.
Kipi kinachomrudisha?
Yanga imeyumba na kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu, ikiwa ni rekodi mbovu kuwahi kutokea miaka ya karibuni. Manji akiwa Mwenyekiti wa Yanga, klabu hiyo ilikuwa na utulivu huku uwanjani ikifanya vizuri kwa kuchukua taji la ligi mara tatu mfululizo, Kombe la FA mara mbili, pia ikitinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mafanikio ambayo yamepotea kwa mwaka mmoja na nusu.
Wapinga kujiuzulu kwake
Gia ambayo kesho itamrudisha Manji ni maamuzi ya mamlaka tatu zenye nguvu ndani ya klabu hiyo kugomea kujiuzulu kwake, baada ya kutangaza Mei 22 mwaka jana. Katika kuachia kwake madaraka huko, Manji alitaja sababu mbalimbali ikiwemo kutoa nafasi kwa wanachama wengine kuiongoza klabu hiyo. Habari hiyo iliwaumiza Yanga na kuona kama wameachwa yatima, vikao vilifanyika na kugomea uamuzi wa Manji huku jitihada zikifanyika kumrudisha.
Kuanzia Kamati ya Utendaji ya Yanga, Baraza la Wadhamini na uongozi wa matawi wote waligomea maamuzi hayo ya Manji.
Anarudi kama nani Yanga?
Haijafahamika Manji akiamua kurudi ndani ya klabu hiyo atarudi kama nani. Mdhamini ama kiongozi, lakini njia ya kurudi kama Mwenyekiti iko wazi kutokana na maamuzi yake ya kujiuzulu kutopewa baraka. Katika mkutano wa kesho wanachama hawatakubali.
Mbali na hayo pia Manji anaweza kurudi Yanga akitafuta nafasi nyingine ingawa uchunguzi unaonyesha endapo atatua mkutanoni anaweza kushindwa kuhimili presha ya wanachama ambao, watamlazimisha kukubaliana na wanalotaka. Ikumbukwe tangu Manji amejiondoa nafasi yake bado iko wazi kwani, uamuzi wake haukupewa baraka hivyo bado anamtambulika kama kiongozi halali.
Msikie Sanga kuhusu Manji
Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alithibitishia Manji ametumiwa mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo, ingawaje alipaswa kuwepo kwa kuwa ni mwanachama hai wa klabu yao. Sanga alisema watafurahi kumuona kwenye mkutano huo, pia uongozi wake hauna kinyongo kwa taarifa za kurejea kwake kwa kuwa nguvu na mawazo yake bado vinahitajika.
“Ukiniuliza akirudi itakuwaje niseme naona katika mitandao, Manji anarudi Yanga wengine wanasema anarudi kwa masharti. Lakini, niseme Manji kurudi Yanga kuna faida na hata kuomba kujiuzulu kwake kama viongozi na wanachama tulipinga maamuzi yake.
“Nguvu ya Manji na hata mapenzi yake kwa klabu ni makubwa, unaweza kuangalia wakati akiwa hapa na hata alipokosekana tulikuwaje na sasa tuko wapi nafikiri tusubiri kuona kipi kitatokea siku ya mkutano Jumapili (kesho).”
Mshindani pekee wa MO
Simba ina maisha safi na kesho inacheza fainali ya Kombe la Sportpesa, utulivu wao umetokana na uwepo wa Mohamed Dewji ‘MO.’ Wana Yanga wanaona katika kipindi ambacho klabu yao imeyumba kifedha mtu pekee anayeweza kushindana na MO ni Manji na endapo atarejea klabuni hapo, basi kila kitu kitakuwa ni freshi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here