Mahakama yaamuru mawili kesi Simba

0
7

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeiondoa hati ya kukamatwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba,

Zacharia Hans Poppe na Franklin Lauwo na imeuamuru upande wa Jamhuri ama kubadili hati ya mashtaka au kuwaondoa washtakiwa ambao hawajakamatwa katika mashitaka ya kughushi nyaraka za kutakatisha fedha yanayowakabili viongozi wakuu wa klabu hiyo.
Kadhalika mahakama hiyo imetoa siku 10 kwa Jamhuri kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka ili kesi iweze kusikilizwa dhidi ya rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu.
Uamuzi huo umetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo baada ya kupitia hoja za utetezi kwamba ili haki iweze kutendeka hati ya mashtaka ifutwe.
“Kuifuta hati ya mashtaka ni dhihaka kwa mahakama,” alisema Hakimu Simba lakini “mahakama hii inatengua hati ya kukamatwa Poppe na Lauwo; upande wa mashtaka uendelee kuwatafuta na ukiwapata una uwezo wa kuwafungulia mashtaka yao.
“Mahakama hii inauagiza upande wa Jamhuri urekebishe hati ya mashtaka kwa kuwaondoa wawili au wafanye mabadiliko ya hati hiyo ndani ya siku 10 ili kesi iendelee.”
Akifafanua zaidi, Hakimu Simba alisema Aveva ni mgonjwa lakini pamoja na kwamba anashindwa kufika mahakamani anasubiri hatma ya kesi yake.
Alisema Aveva na Kaburu walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Septemba 29, mwaka jana na Machi 22, mwaka huu Jamhuri ilidai upelelezi umekamilika.
Hata hivyo, Aprili 30 upande wa Jamhuri uliomba kuwaunganisha washtakiwa hao wawili katika kesi hiyo ambao bado hawajakamatwa na mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa washtakiwa.
Katika kesi ya msingi, Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwamo kula njama ya kughushi na kutakatisha Dola za Marekani 300,000.
Aveva na Kaburu wapo mahabusu tangu Juni 29, mwaka jana kesi hiyo iliposomwa kwa mara ya kwanza kwa kuwa makosa ya utakatishaji fedha hayana dhamana kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here