Yanga wafunguka kilichotokea Algeria

0
8
WAKATI wengi wakihoji sababu ya wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga, usiku wa kuamkia juzi kutovaa jezi zenye nembo ya wadhamini wao, Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa,

Hali iliyozua maswali miongoni mwa wadau wa soka, hatimaye uongozi wa klabu hiyo umefunguka.
Meneja wa klabu hiyo ambayo juzi ilikubali kipigo cha mabao 4-0 mbele ya wenyeji wao, USM Alger ya Algeria, Hafidh Saleh, aliliambia Spoti kwa njia ya simu kuwa walilazimika kuvaa jezi zisizokuwa na nembo ya wadhamini baada ya mawasiliano baina ya klabu hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuchelewa kuwafikia.
Saleh, alisema CAF wana utaratibu wao ambapo klabu inatakiwa kuwasilisha wadhamini wao na Yanga walifanya hivyo, lakini majibu kutoka CAF yalichelewa kuwafikia.
“Mawasiliano hayakuwa mazuri…, lakini kwenye michezo ijayo tutavaa nembo za wadhamini wetu,” alisema Saleh.
Kwa upande wao SportPesa, walisema wanafahamu kuna utaratibu na sheria za CAF zilizosababisha kutovaliwa nembo yao.Afisa Habari wa Kampuni hiyo, Sabrina Msuya, alisema SportPesa bado ni wadhamini wa klabu hiyo.
“Sisi bado ni wadhamini wa Yanga, kuna sheria za CAF ambazo ziliwafanya Yanga wakashindwa kuvaa jezi hiyo na tunalielewa hilo,” alisema Sabrina.
Mwaka 2016, Yanga pia ilicheza michezo yao bila kuvaa jezi za mdhamini walipokuwa wakishiriki michuano hiyo.
Katika mchezo huo, uliochezwa usiku wa kuamkia jana, Yanga bila kuwa na mastaa wake wa kikosi cha kwanza walikubali kipigo hicho kikubwa katika mchezo wao wa kwanza hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa utajiri mkubwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Nyota waliokosa mchezo huo ni pamoja na Kelvin Yondani, Ibrahim Ajibu, Papy Tshishimbi na Obbrey Chirwa.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kushika mkia kwenye kundi lao huku USM Alger wakishika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi tatu wakifuatiwa na Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sport ya Rwanda zenye pointi moja kila mmoja baada ya kutoka sare kwenye mchezo wao.
Yanga itarejea nchini kesho kujiandaa na mchezo dhidi ya Rayon Sport utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Mei 16, mwaka huu.
Credit: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here