Wachezaji wengi wa VPL wanaidharau sana Ligi yetu ya ndani

0
4
NINAMFUATILIA Abdi Banda kila siku pale katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini. Inashangaza sana. Ni mmoja kati ya wachezaji wenye nidhamu. Usishangae sana. Hana kadi nyekundu hata moja.
Huwa anapewa kadi za njano kwa nadra sana.
Hapa kwetu alikuwa mkorofi. Alikuwa mbabe. Aliwahi kupewa kadi nyekundu kwa kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavila bila ya uwepo wa mpira katika pambano kati ya Simba na Kagera Sugar. Mabosi wa TFF wakawa wanaulizana namna ya kumfungia.
Wachezaji wetu hawaheshimu sana ligi yetu. Huwa wanacheza kisela. Mfano mzuri ni namna ambavyo Banda hapati kadi za kijinga pale Afrika Kusini. Kule Afrika Kusini hata Juma Nyosso angeweza kuwa na nidhamu nzuri tu na asifanye mambo anayofanya hapa.
Kule wachezaji wetu wanajua kwamba hakuna mambo ya Simba na Yanga. Wenye ligi yao wanafuata kanuni na taratibu. Hawajali jina la mchezaji wala jina la ukubwa wa timu ambayo anachezea. Hawa kina Banda wanarudi katika mstari kwa kutazama tu mambo yanavyokwenda. Hawana haja ya kuambiwa kwamba uhuni wa Ligi ya Tanzania hauwezi kuupeleka Afrika Kusini au kwingineko.
Hapa kwetu kuna mpira wa kisela. Wachezaji wa Simba na Yanga huwa wanacheza wanavyojisikia na ni nadra sana kupewa kadi nyekundu, hasa wanapocheza na timu ndogo.
Kwa mfano, si ajabu Hassan Kessy asingeonyeshwa kadi nyekundu kama rafu ile angecheza dhidi ya mchezaji wa Mbeya City.
Presha ilimpanda mwamuzi kwa sababu ilikuwa mechi dhidi ya Simba. Kumbe ilikuwa ni kadi halali ambayo ingeweza kutolewa kwa Kessy katika mechi yoyote ya soka kwingineko. Haikunishangaza kuona Kessy alichelewa kutoka uwanjani. Hakuamini kama anastahili kupewa kadi nyekundu.
Katika mechi ya kimataifa mambo mawili yangeweza kutokea. Inawezekana Kessy asingecheza rafu ile, au inawezekana baada ya kupewa kadi nyekundu, basi asingelalamika vile na kugoma kutoka. Pale alijua kwamba Yanga walikuwa wanamsapoti.
Kelvin Yondani naye ni vivo hivyo tu. siku zote anacheza kibabe. Bahati nzuri mate yake yalinaswa na kamera ya Azam TV lakini mara zote Kelvin yupo vile katika mechi za ndani. Mechi za nje huwa anatulia na kucheza kwa amani kwa sababu waamuzi ni makini na hawajui habari za Simba na Yanga.
Mchezaji mwingine mbabe uwanjani ni Juuko Murshid. Anacheza kibabe na rafu za ovyo lakini ni nadra kuona akitolewa nje kwa kadi nyekundu. Mara pekee niliyomuona akitolewa nje kwa kadi nyekundu ilikuwa pale Shinyanga katika pambano dhidi ya Mwadui FC.
Sijawahi kumuona Juuko akicheza ovyo katika mechi za timu ya Taifa ya Uganda ambapo yeye ni mmoja kati ya mabeki wanaopangwa mara kwa mara. Kule anatumia akili zaidi, hachezi rafu, anatawaliwa na busara. Amewakaba hata kina Mohamed Salah lakini bila ya kucheza soka la kibabe.
Kassim Chona wa Prisons ni mbabe mwenzao, lakini kila siku anaambulia kadi nyekundu. Hakuna anayemjali sana kwa sababu hata akipewa kadi nyekundu bado haiwezi kusimama katika kurasa za mbele za magazeti yetu na wala hatuwezi kuhoji maamuzi ya mwamuzi.
Wachezaji wetu wanaidharau ligi yetu. Hawana hofu sana ya kufanya mambo mengi ya kijingajinga kwa sababu wanajua wanalindwa sana. Waamuzi wana hofu na wao. Wachezaji wa Simba na Yanga muda mwingi wanasimama juu ya sheria.
Kadi ya Kessy ndio kadi nyekundu pekee ambayo imetoka kwa mchezaji wa Yanga msimu huu. Kwa upande wa Simba naambiwa hakuna mchezaji aliyepewa kadi nyekundu. Usidhani kuwa wachezaji wao ni malaika, hapana, wana sheria nyingine zinazowasimamia. Wakati mwingine sio suala la kulindwa katika rafu tu. Ni ngumu pia kuona timu nyingine ikipewa penalti dhidi ya Simba au Yanga. Waamuzi wanabebwa na hofu kubwa. Lakini hawa watani huwa wanapewa penalti za kutosha tu. Chunguza katika mechi za watani dhidi ya vibonde. Tahadhari ya mabeki wao inakuwa ndogo zaidi na wanajua waamuzi hawawezi kuchukua maamuzi magumu dhidi yao. Waulize wachezaji wa mikoani wakwambie jinsi wanavyopata ugumu kucheza mechi za Simba
Source: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here