Tanzania Prisons yashikilia ubingwa wa Yanga, Simba

0
10
Dar es Salaam. Ukipiga hesabu, ubingwa wa Simba na Yanga kuvuliwa taji hilo, katikati yao iko Prisons inayocheza na Yanga leo kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Iko hivi. Yanga inacheza na Prisons lakini itakuwa habari mbaya kwao endapo itafungwa au kutoka sare ambayo itakuwa ni habari njema kwa Simba.
Kwa Prisons kuna mawili, endapo itaifunga Yanga au sare itaivua Yanga ubingwa lakini cha pili hali hiyo itakuwa imeipunguzia kazi Simba kwani itatangazwa bingwa wa Ligi Kuu huku ikiwa na mechi tatu mkononi.
Yanga ikipoteza kwa Prisons na ikashinda mechi zake zote zilizobaki, itafikisha pointi 63 na ikitoka sare itakuwa na pointi 64 ambazo tayari zimevukwa na Simba ambayo ina pointi 65 hivyo moja kwa moja Simba kutangazwa bingwa.
Endapo Yanga itashinda, itailazimisha Simba kukaza buti kwa mchezo wake na Singida United, Jumamosi. Simba inahitaji pointi mbili tu itangazwe bingwa.
Yaunganisha safari
Yanga inacheza na Prisons ikiwa imepoteza matuamini ya kutetea ubingwa na tayari kocha Mkongo, Mwinyi Zahera ameipa Simba taji hilo.
Zahera alisema anaelekeza nguvu katika mashindano ya kimataifa ambayo hata hivyo nako Yanga ilianza vibaya kwa kutandika mabao 4-0 na USM Alger mchezo wa kwanza Kombe la Shirikisho.
Mabingwa hao wa Tanzania wako Kundi moja na USM Alger ya Algeria, Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sport ya Rwanda.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Rayon Sports kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya makundi Mei 16.
Wakati Yanga wakiingia uwanajani leo, Simba waliondoka jana jijini Dar es Salaam kwenda Singida, lakini watapitia Dodoma Bungeni kutoa zawadi kwa wabunge mashabiki wa Simba.
Hata hivyo, harufu ya mpambano huo wa Singida na Simba umeanza kwani kocha wa Singida, Hans Pluijm amesema Simba hawatoki.
“Simba hawawezi kutupiga nje, ndani, lazima tutawafunga tu wakitua Namfua,” alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga.
Simba kujazwa noti
Wakati Pluijm akipiga mkwara, wachezaji wa Simba wanatarajiwa kubadili maisha yao kwani wameahidiwa mamilioni endapo tu wataifunga Singida.
Simba itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Namfua kuikabili Singid katika mchezo ambao timu hiyo ikishinda tu, inatangazwa bingwa mpya wa Ligi Kuu msimu huu.
Vigogo wa klabu hiyo wameandaa sherehe kamambe itakayoambatana na zawadi kwa wachezaji wa kikosi hicho.
Habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa vigogo wa Simba ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa klabu, alisema mfadhili wa zamani wa klabu hiyo Mohammed Dewji ‘MO’ anatarajiwa kutoa zawadi ya mamilioni kwa wachezaji.
Chanzo hicho kilidokeza Dewji anatarajiwa kutoa Sh500 milioni endapo Simba itashinda mchezo wa Jumamosi.
Fedha hizo zinatarajiwa kugawanywa kwa wachezaji wote wa kikosi hicho na benchi la ufundi baada ya kutwaa ubingwa.
Mbali na mamilioni ya MO, wachezaji wa timu hiyo wanatarajiwa kugawana fedha ya zawadi ya bingwa wa Ligi Kuu zaidi ya Sh84 milioni.
Simba ina idadi ya wachezaji 29 na benchi la fundi watu saba, hivyo mgawanyo wa fedha zote, kila mmoja anatarajiwa kupata takribani Sh20 milioni.
“MO amewaambia wachezaji wa Simba mbali na ile Sh100 milioni aliyowapa baada ya kuifunga Yanga, atatoa mara tano ya fedha hiyo kwa wachezaji endapo watashinda mechi ya Singida United.
“Pia MO ametuambia kama tukitwaa ubingwa pesa ambayo ni zawadi ya ubingwa zaidi ya shilingi 84 milioni wachukue wachezaji na benchi la ufundi wagawane sawa,” alisema kigogo huyo.
Simba imebakiwa na mechi mbili baada ya kucheza na Singida United, dhidi ya Kagera Sugar na Majimaji ya Songea.
Akizungumza jana, Kaimu Makamu wa Rais Simba, Idd Kajuna alipoulizwa kuhusu fedha hizo alisema Kamati ya Utendaji inatarajiwa kukutana kupanga motisha kwa wachezaji baada ya kutwaa ubingwa.
Kwa upande wake Msemaji wa Simba Haji Manara alipoulizwa, naye alisema motisha itazungumzwa baada ya mchezo dhidi ya Singida United kwa kuwa akili yao inaelekezwa huko.
Credit: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here