Straika mtogo awalainishia Yanga

0
10
Mtogo, Djako Arafat
STRAIKA Mtogo, Djako Arafat ambaye aliwalaza Yanga na viatu waliporudiana na Wolayta Dicha nchini Ethiopia amewaita rasmi mezani kwa kuwatajia thamani yake.
Mchezaji huyo maarufu kwenye Ligi ya Ethiopia mpaka sasa amepachika mabao sita huku mfungaji anayeongoza akiwa nayo kumi huku wachambuzi wa soka la nchini wakidai anashindwa kutupia zaidi kwa vile kikosi kina wachezaji wa kawaida.
Ingawa Yanga inatajwa kukabiliwa na ukata mkubwa kiasi cha kushindwa kulipa mishahara mpaka baadhi ya wachezaji wakagoma, vigogo wake wa usajili walifanya mazungumzo ya awali na Djako baada ya kumalizika kwa mechi ya marudiano ambapo mchezaji huyo mwenye rasta alikuwa na nyota wa mchezo kwa wenyeji kwa kufunga bao 1-0.
Mchezaji huyo alizungumza na Spoti Jumatano, jana Jumanne kutoka nchini Ethiopia na kusisitiza kwamba watu wa Yanga walimwambia kwamba watamcheki ili wamalize dili lakini anashangaa hajapata simu yao mpaka sasa.
Lakini akasisitiza kwamba itafika wakati atafanya maamuzi anayoyajua yeye kwa vile mpaka sasa ana ofa nne mkononi na ya Yanga kama ikimfikia ni ya tano.
“Nilizungumza nao kidogo baada ya ule mchezo lakini wakaniambia watawasiliana na mimi, kuna kitu tunajaribu kukifanya lakini bado hakijakaa sawa, pande zote mbili hazijakubaliana yaani mimi na wao.
“Nina ofa kama nne mezani ninaangalia wapi pa kwenda, ninatafakari kwanza. Yanga wakija na ofa nzuri mimi nasaini muda wowote naangalia zaidi dau linalokuja,” alisema mchezaji huyo ambaye Championi linajua kwamba ana ofa mbili nchini Misri na moja Afrika Kusini lakini hajaamua.
Alipoulizwa kama anataka Yanga wampe bei gani alijibu; “Wakija na dola 150,000 (Sh340m) kwa mwaka nitawapa umuhimu wa kwanza.” Lakini akasisitiza kwamba kama Yanga watakuwa siriazi dau hilo linazungumzika.
Mchezaji huyo ambaye kwa mujibu wa rekodi zake ana miaka 29, alijiunga na Woylata akitokea Awassa ya hapohapo Ethiopia. Alianzia soka kwenye Ligi Kuu ya Ghana katika Klabu ya Ashanti Gold baadaye akauzwa Israel ambako amecheza kwenye klabu mbili tofauti kwa miaka minne kisha akatokomea Arabuni alikodumu kwa msimu mmoja.
Straika huyo aliporudi kwao Togo akapata dili ya Ethiopia ambapo msimu wa kwanza akachachafya na Awassa kabla ya kutua Woylata na sasa anasikilizia dili la Yanga.
Hatahivyo, Yanga wakifanikiwa kukamilisha dili la mchezaji huyo hawataweza kumtumia msimu huu itabidi asubiri msimu ujao kwani hata kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho usajili wao umejaa.
Yanga imesajili wachezaji 30 kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Wilfred Kidau na hawana nafasi ya kuongeza mpaka usajili mpya utakapofunguliwa.
Credit: Global Publsihers

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here