Simba yaionya Singida United

0
9
LICHA ya kuhitaji pointi chache ili itwae ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, wachezaji na benchi la ufundi la Simba wameitahadharisha Singida United kuwa ijiandae kupokea “kichapo” katika mechi itakayowakutanisha keshokutwa kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.

Singida United na Simba ambazo zote zinadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, zinakutana katika mechi ya raundi ya 28 huku wenyeji wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, aliliambia gazeti hili jana kuwa, kwao kila mechi ni sawa na fainali na hawatapunguza “spidi” mpaka watakapofika mwisho wa msimu.
Djuma alisema mbali na kuweka malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu, pia watafurahi kuona wanaweka rekodi ya kutofungwa na kuchukua tuzo mbalimbali zitakazotolewa.
“Msimu una mechi 30, tumecheza 27 na zimebakia tatu, nazo tunataka kushinda na tunajiandaa kama tulivyokuwa tunajiandaa katika mechi zilizopita, mazoezi na nia yetu ni kutopoteza mchezo hata mmoja,” alisema kocha huyo raia wa Burundi.
Mshambuliaji wa timu hiyo, Shiza Kichuya, alisema kuwa wao hawafikirii pointi mbili zinazotajwa kimahesabu na wanajipanga kuchukua pointi tisa za mechi tatu zilizobakia ambazo ni dhidi ya Singida United, Kagera Sugar na Majimaji FC.
” Tunaziwaza pointi tisa na si mbili wanazozisema, hatutabweteka, tunaenda kusaka ushindi na tunataka kuweka rekodi ya kutofungwa,” alisema Kichuya.
Naye Kocha Mkuu wa Singida United, Hans van der Pluijm, alisema kuwa anaifahamu Simba na hataki kuona timu yake inapoteza tena mechi dhidi ya vinara hao.
Pluijm alisema kuwa anajua Simba ina “kiu” ya ubingwa, lakini wachezaji wake pia wanataka kuweka heshima ya kutofungwa mechi zote mbili na kikosi hicho kilichopo chini ya Mfaransa Pierre Lechantre.
Credit: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here