Simba kutangazia ubingwa Singida

0
7
  •  ***Okwi avunja rekodi ya Bocco, sasa amtafuta Tambwe…
BAO pekee la dakika ya 43 kupitia kwa Emmanuel Okwi dhidi ya Ndanda FC, limeifanya Simba kubakiza pointi mbili tu kabla ya kutangazwa bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18, huku likimfanya straika huyo raia wa Uganda kuvunja rekodi ya John Bocco msimu wa 2011/12.
Emmanuel Okwi (Wa Pili Kushoto), Akishangilia Bao Pekee Aliloifungia Simba Wakati Ikishinda 1-0 Dhidi Ya Ndanda Fc Kwenye Mechi Ya Ligi Kuu Iliyopigwa Uwanja Wa Taifa Jana. Kutoka Kulia Ni John Bocco, Shiza Kichuya Na Kushoto Ni Shomari Kapombe. Hilo Ni Bao La 20 Kwa Okwi Msimu Huu. Picha: Bin Zubeiry
Okwi sasa amefikisha mabao 20, hivyo kumpiku Bocco ambaye msimu wa 2011/12 alifunga mabao 19 wakati akiichezea Azam, kilichobaki kwa Mganda huyo ni kuisaka rekodi ya Amissi Tambwe ya mabao 21.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa Taifa jana, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, matokeo ambayo yanaifanya kuendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 65.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuhitaji ushindi dhidi ya Singida United kwenye mechi ijayo itakayopigwa Uwanja wa Namfua mjini Singida mwishoni mwa wiki ili kutangazwa bingwa rasmi wakati ikiwa na mechi mbili mkononi.
Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, ina pointi 49 baada ya kucheza mechi 27 sawa na Simba, kufuatia jana kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Stand United katika mechi iliyopigwa Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
Hivyo endapo Azam itashinda mechi zake tatu zilizobaki itafikisha pointi 58, wakati Yanga yenye pointi 48 baada ya kushuka dimbani mara 24, ikishinda zote zilizosalia itafikisha pointi 66, jambo ambalo linaifanya Simba endapo itashinda mwishoni mwa wiki dhidi ya Singida United kufikisha pointi 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
Katika mechi hiyo, Okwi alifunga bao hilo kwa shuti kali baada ya kuwahadaa mabeki wa Ndanda kufuatia kupokea pasi safi ya Shomari Kapombe.
Mchezo wa jana, Ndanda pamoja na kufungwa walicheza soka safi, lakini umakini mdogo kwenye safu yao ya ushambuliaji iliwakosesha mabao.
Simba wanatakiwa kujilaumu wenyewe kwa kupata ushindi mdogo baada ya nyota wake, Okwi, Bocco na Shiza Kichuya kupoteza nafasi katika vipindi vyote vya mchezo.
Dakika ya 79, Bocco alifunga bao hata hivyo lilikataliwa na mwamuzi baada ya kibendera cha mwamuzi msaidizi kuwa juu kuashiria alikuwa ameotea.
Aidha, matokeo hayo ni mabaya zaidi kwa Ndanda FC inayojipinda kujikwamua kushuka daraja msimu huu.
Kipigo cha jana kwa Ndanda ni cha pili msimu huu baada ya awali kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Simba katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara mabao yote yakifungwa na nahodha wa Simba, Bocco.
Credit: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here