Rooney, Pickford wang’ara tuzo za ‘Dixies’ SportPesa

0
3
WACHEZAJI wa Everton, Jordan Pickford na Wayne Rooney, wameng’ára vilivyo katika tuzo maalum za mwisho wa msimu za klabu hiyo maarufu kama The Dixies baada ya kujizolea tuzo zaidi ya moja kila mmoja.

Mlinda mlango, Jordan Pickford (24), aliibuka kinara kwenye tuzo hizo zilizofanyika Mei Mosi, mwaka huu kwenye ukumbi maarufu wa Liverpool, Philharmonic baada ya kutwaa tuzo tatu kwa mpigo za Mchezaji Bora wa Msimu, Mchezaji Chipukizi na Mchezaji Bora Chaguo la Wachezaji wenzake.
Pickford ambaye amesajiliwa na Everton kwa dau lililoweka rekodi kwa makipa wa Kiingereza kwenye EPL, akitokea Sunderland msimu uliopita, amefanikiwa kuanza kwenye mechi zote 36 za Everton msimu huu za Ligi Kuu, huku akicheza mechi 10 bila kuruhusu bao na kuokoa jumla ya michomo 116.
Bao Bora
Katika tuzo hizo ambazo zimefanyika kwa msimu wa pili mfululizo tangu kuanzishwa kwake mwaka jana, Rooney amefanikiwa kuchomoka na tuzo mbili.
Rooney (32), ambaye ni mfungaji bora wa Everton kwenye msimu huu wa 2017/18 wa EPL akiwa na mabao 10, amefanikiwa kutwaa tuzo ya Bao Bora la Msimu alilofunga dhidi ya West Ham kwa umbali wa mita 59.
Rooney pia ametwaa tuzo ya Kiwango Bora kuonyeshwa na mchezaji kwenye mechi moja ambayo ameitwaa kupitia mechi hiyo hiyo ya West Ham ambapo Everton walifanikiwa kushinda kwa mabao 4-0 huku akitupia hat-trick.
Wachezaji wengine ambao walifanikiwa kutwaa tuzo kwenye usiku huo ni pamoja na mlinzi wa kulia wa klabu hiyo, Seamus Coleman huku wakongwe Phil Jagielka na Leighton Baines nao hawakusahaulika baada ya kila mmoja wao kutwaa tuzo ya Howard Kendall ikiwa ni shukrani kwa mchango wao mkubwa kwenye klabu hiyo ambayo wamedumu kwa miaka 11 tangu waliposajiliwa mwaka 2007.
Chimbuko
Tuzo hizo za heshima zimepewa jina la mshambuliaji wa zamani wa Everton na timu ya Taifa ya England, William Ralph Dean maarufu kama Dixies ambaye aliichezea Everton mwaka 1925-1937 akifunga zaidi ya mabao 300.
Chanzo: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here