Ngoma, Tambwe waitesa Yanga

0
7
  • ***Uongozi waogopa mkono wa sheria kuwakata, wasema…
UONGOZI wa Yanga umekiri kuwa suala la mkataba kati ya wachezaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe, ndilo linalosababisha klabu hiyo kushindwa kuwatema licha ya kutotumika kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.
Ngoma na Tambwe wameshindwa kuichezea timu yao msimu huu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, aliliambia gazeti hili kuwa wanatakiwa kuwa makini katika kukatisha mikataba ya nyota hao ili kukwepa kuangukia pabaya kisheria. 
Alisema kukatisha mikataba na wachezaji hao kwa sasa, kutailazimu Yanga kuwalipa wachezaji hao raia wa Zimbabwe na Burundi.
“Lazima kuwe na umakini na si jambo la kukurupuka kuwakatishia mikataba, ni kweli hawajacheza kwa muda mrefu, lakini klabu haiwezi kukurupuka kukatisha mikataba yao,” alisema Mkwasa.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kwa sasa inapitia katika kipindi kigumu kutokana na nyota wake kuwa majeruhi wakati huu ikikabiliwa na kazi ngumu ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara na kibarua kigumu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mabingwa hao watetezi wamezidiwa kwa pointi 17 na vinara Simba kwenye msimamo wa Ligi Kuu, lakini ina mechi tatu mkononi, wakati huu ‘Wekundu wa Msimbazi’ hao wakiwa wamecheza michezo 27 na kujikusanyia pointi 65.
Yanga ambayo Alhamisi itashuka dimbani kuivaa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, ilitarajiwa kurejea nchini jana kutoka Algeria ilipokwenda kucheza mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger.
Katika mchezo huo uliochezwa Jumapili iliyopita, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 4-0.
Chanzo: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here