Lechantre Abakisha Saa 648 Tu Simba Sc

0
11
WAKATI kesho Simba ikicheza na Ndanda FC, kocha wake mkuu Mfaransa, Pierre Lechantre amebakisha siku 27 sawa na saa 648 za kubaki kuendelea kukinoa kikosi hicho.
Simba inayoongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 62, inatarajiwa kuvaana na Ndanda katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo alitua nchini Januari 16, mwaka huu akiwa na kocha wa viungo Mmorocco, Mohammed Aymen Hbibi kwa ajili ya kumrithi aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon aliyetimuliwa.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Lechantre alithibitisha mkataba wake kumalizika mwezi ujao huku kukiwa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika juu ya mkataba wake mpya wa kubaki kuinoa Simba.
Lechantre alisema, wakati ligi ikielekea ukingoni hawezi kuzungumzia mikakati ya usajili ya msimu ujao wa ligi kutokana na kutojua hatma yake katika timu hiyo huku wakiwa wamebakiwa na mechi nne tu.
Kocha huyo alisema atazungumzia mikakati ya timu yake ikiwemo mapendekezo ya usajili wa wachezaji wapya na ambao mikataba yao inaisha wakiwemo Shiza Kichuya, Said Ndemla na Mohamed Ibrahim ‘Mo’ baada ya yeye kusaini mkataba mpya.
“Nina mipango mingi na Simba na moja kati ya hiyo ni kuijenga Simba itakayokuwa imara na kuleta ushindani wa kitaifa na kimataifa katika msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa.
“Kama nikifanikiwa kuongezewa mkataba mpya, nakuhakikishia Simba itakuwa tishio, hivyo kwa hivi sasa siwezi kuweka malengo na mikakati yangu ndani ya Simba ikiwa mkataba wangu unaelekea kumalizika mwezi ujao na kama unakumbuka nilisaini mkataba wa miezi sita wakati ninajiunga na Simba.
“Sitakuwa katika sehemu nzuri ya kupendekeza wachezaji wapya wa kusajiliwa na wale wa zamani kuongezewa mikataba kama sitaongezewa mkataba wa kuendelea kuifundisha Simba.
“Kocha anapendekeza wachezaji wale wazuri atakaoona anaweza kufanya nao kazi watakaoendana na mfumo wake na si nje ya hapo,” alisema Lechantre.
Akizungumzia ishu hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba mwenye ushawishi mkubwa, Said Tully alisema; “Kwa sasa tunafikiria zaidi mechi za ligi ili tutwae ubingwa halafu tutarudi katika mambo ya mikataba.”
Credit: Global Publishers

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here