Kumbe Okwi alijipanga mapema unaambiwa

0
4
KINARA wa mabao Ligi Kuu Bara, Emmanuel Okwi, aliyeifungia Simba mabao 20 hadi sasa, ameweka wazi namna alivyokuwa amejipanga msimu huu na kile kilichotokea.
Okwi aliyewahi kutamba na Yanga na SC Villa ya Uganda, alisema alijiwekea malengo mawili msimu huu ambayo ni kutwaa ubingwa ambao wameshafanikiwa kwa asilimia tisini na pia kufunga mabao 30 katika mashindano yote.
“Naomba niseme kwa mara ya kwanza hapa Mwanaspoti kwa sababu ni moja ya gazeti ambalo naliamini. Msimu huu nilipanga kufunga mabao 30, katika mashindamo mawili ambayo ni Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu,” alisema Okwi aliyewahi kucheza soka la kulipwa nchini Tunisia na Denmark.
“Kwenye Shirikisho nimefunga matatu, lakini hatukupata bahati ya kuendelea na kama tungepata nafasi ya kuendelea katika hatua inayofuata ningekuwa na uwezo wa kufunga zaidi ya hayo.
“Katika malengo yangu ya kufunga si mbaya kwani nadaiwa mabao saba ili kufikia yale 30. Nimejiwekea dhamira katika mechi hizi tatu ambazo tumebakiza nifunge zaidi hivyo kama nitaweza kufunga idadi hiyo nitafurahi sana,” alisema Okwi aliyesajiliwa na Simba kwa mara ya kwanza mwaka 2009.
Simba wamebakiwa na mechi tatu ambazo ni dhidi ya Singida United, itakayopigwa Jumamosi hii pale Namfua Singida, kisha Kagera Sugar kabla ya kuifuata Majimaji mjini Songea.
Akizungumzia rekodi ya mabao mengi Ligi Kuu iliyowekwa na nyota wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ miaka 20 iliyopita alipofunga mabao 26, Okwi alisema kwanza alikuwa anataka kuisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ambao wanausaka kwa muda mrefu halafu baada ya hapo ni kuangalia jinsi gani anaweza kufanya vizuri kama mchezaji.
“Nafahamu kuna rekodi ya Mmachinga aliyewahi kufunga mabao 26, katika msimu mmoja na nimebakiwa na mechi tatu ambazo nitajituma kama naweza kufunga nikafikia rekodi hiyo au kuivunja itakuwa vizuri,” alisema.
“Kuvunja rekodi si kitu kibaya ni jambo zuri kwa mchezaji kuongeza hali ya kujiamini na thamani yako ndani ya klabu,” alisema Okwi ambaye usajili wake kabla ya msimu kuanza ulibezwa na wapinzani wakisema ni mchezaji mzee aliyeisha makali.
Credit: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here