Kocha Zahera amkacha Mfaransa

0
2
UNAWEZA kudhani ni utani, ila ndio ukweli ulivyo kuwa mashabiki wa Simba na Yanga huwa hawawezi kukaa jukwaa moja, tena kila mmoja akiwa na jezi ya timu yake.
Hakuna anayejua sababu ya jambo hilo, ila ndivyo imezoeleka kwenye viwanja vyetu vya soka na kama ikitokea mmoja akajichanganya kwa wenzake, basi hupata kashkashi wakati mwingine hata kuambulia kipigo. Imeshuhudiwa mara kadhaa jambo hili.
Lakini sasa, jambo hilo kwa makocha wa timu hizo wala huwa halisumbui sana, kwani mara kadhaa wamekuwa wakigongana na kuishi katika hoteli moja na mambo yakaenda poa ikiwamo kupiga stori mbili tatu kirafiki bila kununiana.
Ni kama ishu ilivyokuwa kwa makocha wa sasa wa timu hizo, Mkongomani Mwinyi Zahera na Mfaransa Pierre Lechantre, wote walijikuta wakibana hoteli moja na nyakati fulani fulani walikuwa wakipiga stori mbili tatu kabla ya mmoja kuamua kumkacha mwenzake.
Iko hivi. Kocha wa Simba, Lechantre anaishi hoteli moja ya maana ya Seascape kule Mbezi Beach sehemu ambayo amekaa tangu afike nchini kuanza kuifundisha timu hiyo.
Yanga nayo baada ya kocha wake Mzambia George Lwandamina kutimka iliamua kumleta raia wa DR Congo ambaye pia ana uraia wa Ufaransa, Mwinyi Zahera na kumpeleka hoteli hiyo hiyo bila mmoja kujua lolote.
Wawili hao baada ya mchezo wa Simba na Yanga wakakutana katika mgahawa wa hoteli hiyo wakienda kupata kifungua kinywa na kuanza kutoleana macho kila mmoja akimshangaa mwenzake kisha kupotezea na kuanza kupiga stori mbili tatu.
Aliyefichua hayo ni Kocha Zahera, aliyeliambia Mwanaspoti alikutana na Lechantre wakati wakitaka kupata kifungua kinywa kisha kila mmoja alitumia sekunde chache kukumbuka ameonana wapi na kugundua kumbe walionana Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Yanga ililala 1-0 kwa Mfaransa huyo.
Zahera alisema alipokutana na Lechantre hakukuwa na tofauti yoyote kwani walitambulishana na kupiga stori mbili tatu za soka hapa nchini hususani mchezo baina yao kisha kuhamishia stori za Ufaransa.
Hata hivyo, Zahera alisema aliporudi nchini akitokea Algeria alilazimika kuhama hoteli hiyo bila kumuaga Lechantre baada ya kufika hotelini hapo na kukuta imejaa akiambiwa Simba imeweka kambi hapo ambapo alilazimika kuhamia hoteli nyingine.
“Namjua Lechantre, lakini nimemfahamia hapa Tanzania, nilimuona uwanjani siku ya mchezo na baada ya ile mechi nikaja kumuona hotelini wakati nataka kupata kifungua kinywa,” alisema Zahera.
“Nilianza kujiuliza huyu nimewahi kumuona wapi na baadaye kikakumbuka kumbe ni pale Taifa.
“Ni mtu mzuri tulibadilishana mawazo, lakini pia nilimpongeza kwa kushinda ile mechi. Hata hivyo nimehama pale baada ya kukuta pamejaa niliporudi kutoka Algeria, hata hivyo sikumuaga.”
Credit: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here