Failuna awazima Wakenya Mbeya Tulia Marathoni

0
4

  • Failuna aliibuka kidedea baada ya kumaliza mbio za kilomita 21 huku akionyesha ushujaa wa kutopitwa na Mkenya Christina Kambua aliyemaliza katika nafasi ya pili.
Mbeya. Mwanariadha Failuna Abdi ameibuka shujaa wa mbio za Mbeya Tulia marathoni zilizofanyika jana mkoani hapa.
Failuna aliibuka kidedea baada ya kumaliza mbio za kilomita 21 huku akionyesha ushujaa wa kutopitwa na Mkenya Christina Kambua aliyemaliza katika nafasi ya pili.
“Mpinzani wangu alijua nitachoka na yeye atanipita njiani, lakini safari hii sikutaka kupitwa mwishoni, nilipambana mwanzo mwisho hata njiani sikumpa nafasi.
“Alijaribu kutumia mbinu ya kuvuta pumzi akitegemea nitachoka na kuacha mbinu yake ikafeli,” alisema Failuna muda mfupi baada ya kumaliza mbio hizo.
Alisema ushindani ulikuwa mkali, lakini alikuwa na uchungu wa kupitwa na Wakenya, hivyo alipambana kwa nguvu kubwa na kupata ushindi.
Failuna alitwaa medali ya dhahabu na fedha Sh2 milioni, Christina Sh700,00 na Adelina Trazias wa Tanzania aliyemaliza wa tatu alipata Sh500,000.
Kenya ilitawala upande wa wanaume, Bernad Musau aliibuka kinara na kupata Sh2 milioni na medali ya dhahabu.
Paschal Mombo anayenolewa na bingwa wa zamani wa maradhoni katika michezo ya Madola, Gidamis Shahanga alishika nafasi ya pili na kupata Sh700,000. George Olihaki wa Kenya alimaliza wa tatu na kuvuna Sh500,000.
Mnyukano mwingine ulikuwa kwenye marathoni ambapo Sarah Ramadhani aliitoa Tanzana kimasomaso upande wa wanawake baada ya kumaliza wa pili akitumia saa 3:20:53 akiwa nyuma ya
bingwa kutoka Kenya, Beatric Rutto aliyekimbia kwa saa 3:18:32.
“Sijui mshindi alipitia njia gani, lakini hadi tunamaliza kilomita 30 nilikuwa nimemuacha mbali tu, sikumuona akinipita hadi nakaribia kumaliza ndiyo nikamuona mbele yangu,” alisema Sarah.
Emilly Jeekoech wa Kenya aliyekimbia kwa saa 3:27:06 alimaliza wa tatu.
Upande wa wanaume, nyota wa timu ya taifa, Marco Joseph, Said Makula na Dickson Marwa walishindwa kutamba mbele ya Mkenya
Abraham Too aliyetwaa dhahabu akikimbia kwa saa 2:42:02.
Mtanzania John Leonard alimaliza wa pili akikimbia kwa saa 2:42:39
ingawa ushindi wake ulipingwa na Mkenya.
Mbio hizo zilizoteka hisia za mashabiki wa riadha zilianza saa 12:00 asubuhi kwenye Uwanja wa Sokoine zilishindanisha wanariadha wa marathoni (kilomita 42), nusu marathoni (kilomita 21), kilomita tano za wanafunzi, kilomita 21 za walemavu, kilomita mbili za wazee, kilomita tano za kujifurahisha na mbio fupi za uwanja (mita 100 mpaka 800) na mbio za baiskeli za kilomita 150 za wanaume na kilomita 75.
Mbio hizo ambazo ziliandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust zikiwa na lengo la kuchangia fedha kwenye sekta ya elimu na afya nchini. Mbio hizo zilianzishwa mwaka 2016.
Credit: Mwananchi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here