Yanga morali juu kwa Waethiopia

0
3

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania waliobakia kwenye michuano ya kimataifa, Yanga, walitarajia kuondoka nchini leo alfajiri kuelekea Ethiopia kuwafuata wapinzani wao Welayta Dicha FC, wameahidi kupambana na kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi.

Welayta Dicha inatarajia kuikaribisha Yanga katika mechi ya marudiano ya hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa kesho, Jumanne mjini Awassa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa, alisema kuwa wanajua wanaenda katika mapambano na hawatabweteka na ushindi walioupata katika mechi ya kwanza iliyopigwa Aprili 7, mwaka huu na kushinda 2-0.
Nsajigwa alisema anajua wako katika changamoto ya kuondokewa na Kocha Mkuu, George Lwandamina, lakini watahakikisha wanapambana na kupeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa.
Nahodha na beki huyo wa zamani wa Yanga aliongeza kuwa wamewaandaa wachezaji wao kujituma katika mchezo huo na kutoweka kichwani mawazo ya kutolewa katika mashindano ya Kombe la FA na Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Tunajua tulicheza dakika 90 za kwanza na sasa tunaenda kumalizia awamu ya pili, hakuna mechi rahisi, tunaahidi kupambana ili tusonge mbele, hatutabweteka kwa sababu tulishinda mechi ya kwanza na wao wanaweza kugeuza matokeo,” alisema Nsajigwa.
Aliongeza kuwa, anaamini wataimarika zaidi baada ya kurejea kwa nyota wake wa kikosi cha kwanza ambao walikosa mchezo uliopita kwa sababu ya kutumikia kadi tatu za njano.
“Sasa hivi tutaingia na nguvu zaidi kwa sababu mechi ya kwanza hatukuwa na kina Yondani (Kelvin) na Chirwa (Obrey), ila bado tunaomba mtuombee ili tusonge mbele,” Nsajigwa aliongeza.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watashuka uwanjani wakiwa na rekodi ya ushindi wa mabao 2-0, na mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Chanzo: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here