Yanga hesabu kali Ethiopia

0
3
  • ***Inashuka uwanjani kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi michuano ya CAF…
KAZI moja! Wachezaji wa Yanga wameahidi kupambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi ya marudiano ya hatua ya mtoano ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Welayta Dicha FC itakayofanyika leo mjini Awassa, Ethiopia.
Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa ambao wanadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa watashuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0, hivyo wanahitaji sare au ushindi wowote ili wasonge mbele.
Akizungumza na gazeti hili jana, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub “Cannavaro” alisema kuwa mechi ya leo ni muhimu kwao kwa sababu wanahitaji kuingia katika hatua ya makundi na vile vile kupata fedha zinazotolewa baada ya kufika hatua hiyo.
Cannavaro alisema pia wanatarajia kukutana na changamoto kutoka kwa wapinzani wao lakini akitamba kuwa leo kikosi chao kitakuwa kamili baada ya baadhi ya nyota waliokosekana katika mechi ya kwanza akiwamo straika, Obrey Chirwa, kurejea.
“Mawazo yetu yako katika mechi hii ya kimataifa, ni muhimu sasa kuliko kitu kingine kwa wakati huu, tukirejea nyumbani ndiyo tutaanza kuifikiria Simba na vita ya Ligi Kuu kwa ujumla,” alisema beki huyo.
Naye Meneja wa timu hiyo,Hafidh Saleh, alisema kuwa wanamshukuru Mungu wachezaji wote wako katika hali nzuri na wanachosubiri ni muda na siku ya mchezo ifike.
“Maandalizi yako vizuri na kila mchezaji hapa anawaza ushindi na kuvuka hatua hii tuliyopo,” alisema meneja huyo.
Endapo Yanga itatinga hatua ya makundi itakuwa na uhakika wa kupata pesa zinazotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambalo hutoa Sh. bilioni  1.8 kwa timu itakayomaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi huku Sh. milioni 536 zitakwenda kwa klabu zitakazoshika nafasi ya pili na ya tatu huku ile itakayoburuza mkia itapata Sh. milioni 336.
Mara ya mwisho Yanga kutinga hatua ya makundi ilikuwa ni mwaka 2016 ilipokuwa chini ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na ilikuwa kundi moja na TP Mazembe, MC Alger na Medeama FC ya Ghana.
Chanzo: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here