Sakata la Yondani kuwa na kadi mbili za njano kimenuka

0
5Baada ya kupokea barua ya kuonywa kutowatumia wachezaji wake wanne, Yanga imekwenda kwenye Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa kupinga adhabu ya kadi mbili za njano alizopewa nahodha na beki wao wa kati, Kelvin Yondani.

Caf juzi Jumatano iliitumia barua Yanga ikiwaonya kutowatumia wachezaji wake wanne wenye adhabu wa kadi akiwemo Yondani, Obrey Chirwa, Kabamba Tshishimbi na Said Makapu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Waleyta Dicha FC ya nchini Ethiopia utakaopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Shirikisho hilo pia, lilituma barua kwa Dicha likiwatahadharisha kutowatumia wachezaji wao wenye adhabu ya kadi mbili za njano ambao ni Teklu Kumma na Eshetu Medelcho.

Meneja Mkuu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema wamefikia hatua hiyo ni baada ya kupata taarifa za Yondani kuzuiliwa kucheza mechi ya Dichaa kwa kuwa na kadi mbili za njano kitu ambacho siyo sahihi.
Saleh alisema, wanakwenda kupinga adhabu hiyo Caf baada ya yeye kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo kujiridhisha kwa kupitia video za mechi zao walizocheza na kwenye mafaili yao ya kumbukumbu.

Aliongeza kuwa, suala hilo analifuatilia katibu, Boniface Mkwasa ambaye tayari ameanza kufanya mawasiliano na Caf mara baada ya kupokea barua, hivyo wana matumaini makubwa suala hilo kumalizika kwa haraka kabla ya mechi hiyo.
“Tumeshangazwa na hizi taarifa za Yondani kuwa na kadi mbili za njano kitu ambacho siyo kweli, mimi binafsi kama meneja katika mafaili yangu yanaonyesha mchezaji huyo hana kadi mbili, hivyo nashangaa kusikia ana idadi hiyo na kadi na kuwa hataukosa mchezo huo.

“Niwahakikishie Wanayanga kuwa, Yondani ana kadi moja pekee ya njano hivyo nina wasiwasi mkubwa mmoja wa waamuzi alikosea kuandika kumbukumbu zake za kadi kwa kukosea namba ya jezi baada ya kumuandika mchezaji mwingine yeye akuandika Yondani.

“Tayari tumeanza kulishughulikia hilo kupitia kwa katibu wetu Mkwasa ambaye yeye amefanuya mawasiliano na Caf ili kujua jinsi gani kadi ya pili ya Yondani inafutwa na kuwepo katika sehemu ya wachezaji tutakaowatumia katika mechi hii,” alisema Saleh.

SOURCE: CHAMPIONI
Na: Agape Patrick
Email: agape@spoti.co.tz

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here