Okwi, Bocco wasisitiza ubingwa Bara kwanza

0
4
WASHAMBULIAJI wa Simba, Emmanuel Okwi na John Bocco, kwa nafasi tofauti juzi walisema kuwa, wanatumia nguvu zaidi kuisaidia timu yao ipate pointi tatu katika kila mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara na si kufikiria tuzo ya kiatu cha dhahabu.
Okwi amefikisha mabao 19 msimu huu wakati Bocco yeye ana magoli 14, baada ya kila mmoja kufunga katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Prisons ambao timu yao iliupata juzi.
“Kila siku kwanza nawaza kuisaidia Simba ipate ushindi, kwangu malengo ni kutwaa ubingwa na si kiatu cha dhahabu,” alisema Okwi.
Naye Bocco, nahodha wa kikosi hicho kinachoongozwa na Mfaransa, Pierre Lechantre, alisema kuwa kila anaposhuka uwanjani anahakikisha anajituma ili timu yake ishinde bila kujali nani atakayefunga goli.
“Kipaumbele changu huwa ni kuona Simba inapata ushindi, na ndiyo malengo ya timu nzima, na ili kutimiza hili, ninajaribu kupambana kufunga kila ninapopata nafasi, ingawa najua mechi zote tunazocheza ni ngumu,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Azam FC.
Kikosi cha Simba kinatarajia kuingia kambini leo ili kuanza maandalizi ya kuelekea Iringa kuwafuata wenyeji wao Lipuli FC, ambao watawaalika katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara itakayofanyika Jumamosi.
Chanzo: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here