Njaa yaendelea kuitesa Yanga

0
6
WAKATI kikao cha Kamati ya Utendaji cha Yanga kilichofanyika juzi kushindwa kufikia muafaka wa kuteua mrithi wa Kocha, George Lwandamina, viongozi wa klabu hiyo wameshindwa kufikia makubaliano na makocha waliopendekezwa kutokana na kukosa fedha za kuwalipa wanazohitaji, imefahamika.
Baadhi ya makocha ambao walitajwa katika kikao hicho ili kuja kurithi mikoba ya Lwandamina ni pamoja na Kocha wa Mbao FC ya Mwanza, Ettiene Ndairagije na Nsanzurwino Ramadhani wa Mbeya City ya jijini Mbeya.
Akizungumza na gazeti hili jana, kiongozi mmoja wa juu wa Yanga ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa (jina tunalihifhadi) alisema kuwa kila kocha ambaye wamejaribu kuzungumza naye, amewatajia kiasi cha juu cha mshahara ambacho klabu hiyo kwa sasa haina uwezo wa kulipa.
Kiongozi huyo alisema kikao hicho kimekiri kuwa timu yao inahitaji kocha kutoka nje ya nchi ili iweze kupambana na kufanya vyema katika mashindano mbalimbali watakayoshiriki, hivyo suala la kuteua kocha mzalendo kwa sasa haiwezekani.
Alisema pia hata kocha ambaye watamleta, watahakikisha wanampa mkataba mfupi, lakini wakifanya naye mazungumzo ya kuongeza au kusitisha mapema badala ya kusubiri dakika za mwisho za mkataba.
“Lwandamina ameondoka akiwa hajalipwa mshahara, sasa unajiuliza huyu nitakayemleta nitamlipa nini, hili ni moja ya tatizo ambalo linatusumbua kwa sasa, na ili kuepuka aibu hii, hatutatoa mikataba kama ile iliyosainiwa enzi za (alitaja jina la kiongozi) ambayo sasa inatutesa na kutuweka kwenye aibu,” kilisema chanzo chetu.
LWANDAMINA ATAMBULISHWA Taarifa kutoka Lusaka, Zambia zinasema kuwa hadi jana mchana Zesco ilikuwa bado haijamtambulisha Lwandamina kuwa amerejea rasmi katika klabu hiyo.
Lwandamina ambaye aliipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ulipita, anatajwa kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili na timu yake hiyo ya zamani.
Mzambia huyo ameiacha Yanga ikiwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na imeondolewa kwenye mashindano ya Kombe la FA ambayo bingwa wake atashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Chanzo: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here