“Nimejifunza mambo mengi sana Commonwealth”-Mkurugenzi wa michezo,

0
2
Mkuu wa msafara wa wachezaji na viongozi ambao walikwenda Australia kushiriki mashindano ya Jumuia ya Madola ambaye ni Mkurugenzi wa michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Yusuf Singo amesema vitu ambavyo amejifunza kwenye mashindano hayo baada ya Tanzania kurudi mikono mitupu.

Singo amesema kuna haja ya kuangalia aina ya michezo tunayotaka kwenda kushiriki kwenye mashindano ya Jumuia ya Madola kwa sababu kuna baadhi ya michezo itatuchukuwa muda mrefu kuweza kupata medali.

“Nimejifunza mambo mengi, kwanza yale ni mashindano makubwa sana wenzetu wanajiandaa mapema mno, hivi tunavyoongea wenzetu wameanza maandalizi ya Olympic na tulivyomaliza mashindano wenzetu wanaanza maandalizi ya mashindano ya Jumuia ya Madola yanayofuata ambayo yatafanyika Birmingham.”

“Pia nimejifunza ni lazima tuangalie ni michezo gani tukiipeleka tunaweza tukashinda, nimegundua kuna michezo tutafanya kazi ya ziada sana kuja kupata medali.”

“Mashindano yalikuwa magumu, tumeshiriki michezo yote minne wakati mwingine hivi vitu vinakwenda na bahati na ndivyo ilivyotokea. Mchezo wa ngumi mabondia wetu wote hawakufanikiwa kwenda hatua ya pili ilikuwa kama bahati mbaya wengi wao walipangiwa mabondia wenye uwezo mkubwa kwa mfano bondia wetu mpya alipangiwa bondia mtetezi na mwingine alipangwa na bondia wa India ambao kwa sasa ni wazuri sana.”

“Table tennis tulifika hadi robo fainali lakini hatukufanikiwa kusonga mbele. Upande wa riadha (marathon) mkimbiaji wetu mmoja wakati amefika kilometa 41 akiwa wa tatu bahati mbaya alianguka kwa sababu ya hali ya hewa kuwa mbaya kwake hata aliyekuwa anaongoza naye pia alianguka kwa hiyo hatukufanikiwa.”

Posted by Lebab
Source: The Guardian

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here