Mwandila amrithi Lwandamina Yanga

0
6
 Baada ya kocha George Lwandamina kutimkia Zesco United ya Zambia hivi karibuni, uongozi wa Yanga jana umemtangaza Noel Mwandila kuwa kocha mkuu hadi mwisho wa msimu.
Mbali ya Mwandila makocha wengine wenye uwezo wa kuziba pengo la Lwandamina ni Etienne Ndayiragije, Hans Pluijm, Juma Mwambusi, Masoud Djuma na Ally Bizimungu.
Ingawa baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wakimpigia chapuo kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa kupewa jukumu la kusimamia benchi la ufundi la Yanga moja kwa moja lakini imebainika hajafikia vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
Hata hivyo kanuni za Kombe la Shirikisho Afrika ambalo Yanga inakaribia kuingia hatua ya makundi zikielekeza kwamba Kocha Mkuu ni lazima awe na leseni A inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaelekeza kwamba Kocha Mkuu wa timu inayoshiriki ligi hiyo anatakiwa anagalau awe na leseni daraja B ya CAF.
“Kwa msimu wa 2017/2018 Kocha Mkuu wa timu ya kwanza ya klabu ya Ligi Kuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia Daraja B ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya Mabara mengine. Kuanzia msimu wa 2018/2019 na kuendelea Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia Daraja A ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya Mabara mengine yanayotambuliwa na FIFA,” kinafafanua kifungu cha 3 cha kanuni ya 71 ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Nsajigwa ana leseni daraja C ambayo kikanuni haimpi nafasi ya kuwa Kocha Mkuu wa timu kama Yanga.
Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema hawana mpango wa kutafuta kocha mpya kwa sasa.
“Nsajigwa ni kocha msaidizi na itabaki kuwa hivyo wala vigezo vyake havimzuii kukaa benchi kama msaidizi, majukumu ya kocha mkuu kwa sasa yatakuwa chini ya Noel (Mwandila),” alisema Mkwasa.
“Mechi zilizosalia ni chache, hatuoni sababu ya kuleta kocha mpya, tutaajirli kocha mwanzoni mwa msimu ujao,” alisema Mkwasa.
Wanapewa nafasi ya kutua Yanga ni Ndayiragije ambaye siku zake Mbao FC zimeanza kuhesabika kutokana na mfululizo wa matokea yasiyoridhisha ya timu hiyo yaliyochangia mashabiki kutaka kocha huyo ajiuzulu.
Kama hiyo haitoshi, Ndayiragije mwenye leseni daraja B inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), hakuonekana kwenye benchi la ufundi la Mbao FC wakati ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Njombe Mji, Jumatano.
Katika kukoleza fununu za kocha huyo kutua Yanga, Mbao FC kwa sasa imemuongeza Fulgence Novatus ndiye amekuwa akisimamia mazoezi ya timu hiyo.
Akizungumzia taarifa za Yanga kutaka kumchukua Ndayiragije, Mkwasa alisema kwa kifupi kuwa huo ni uvumi.
“Tutana mpango wa kuajirli kocha, lakini siyo sasa na kuhusu kocha wa Mbao kuja Yanga huo ni uvumi tu,” alisema Mkwasa.
Yanga ina uwezekano pia wa kumpata kocha wake msaidizi wa zamani, Juma Mwambusi ambaye kwakwa sasa hana timu tangu alipoachana na mabingwa hao msimu uliopita.
Mwambusi ana leseni A ya ukocha kutoka CAF, anaifahamu vyema Yanga aliitumikia takribani miaka miwili akiwa msaidizi wa Hans Pluijm na baadaye Lwandamina hivyo ana uwezo mkubwa wa mashindano ya ndani na ya nje ingawa pia anabebwa na heshima aliyojijengea kwa wachezaji wa Yanga.
Kocha mwingine anayeweza kuirudisha Yanga katika mstari ni Pluijm wa Singida United kutokana na kocha huyo kuifahamu vyema klabu hiyo baada ya kuinoa kwa nyakati mbili tofauti na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili, kutwaa ubingwa wa Kombe la FA msimu wa 2015/2016 pamoja na kuifikisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016.
Hata hivyo, Yanga ina kibarua kigumu kumnasa Pluijm ambaye ni mwanachama wake kwani italazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumshawishi avunje mkataba wake na Singida United, pia kuna tetezi ameshafikia makubaliano na Azam FC.
Kuhusu kuhusishwa kwake na Yanga, Kocha Pluijm alisema anaheshimu mkataba wake na Singida United. “Siyo Yanga tu bali pia nimekuwa nikihusishwa kujiunga na Azam FC, niseme wazi kwamba nina mkataba na Singida United na akili na malengo yangu ni kuisaidia ifanye vizuri katika mashindano yaliyo mbele yetu na sio kushughulika na hizo habari zinazozushwa,” alisema Pluijm.
Kocha mwingine anayeweza kutua Yanga kwa kipindi hiki ni Ally Bizimungu wa Mwadui FC ameweza kuibadili timu hiyo na kuiondoa kwenye janga la kushuka daraja tofauti na alivyoikuta.
Bizimungu alisema yuko tayari kujiunga na Yanga ikiwa watamhitaji ingawa ni lazima aagane vizuri na Mwadui.
“Binafsi nimekuja Tanzania kufanya kazi hivyo kama nafasi ya kufundisha timu kama Yanga inakuja, ni vigumu kuiacha ipite ingawa hilo litafanyika baada ya kupata baraka za Mwadui.
“Nimesomea ukocha Ujerumani kwa lengo la kuwa kiongozi wa benchi la ufundi na siyo kuwa msaidizi hivyo sharti langu kuu kwa timu yoyote itakayonihitaji ni niwe kocha mkuu,” alisema Bizimungu.
Yanga pia inaweza kujaribu bahati yake kwa kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma aliyeonyesha uwezo wa hali ya juu wa kusimamia timu kutokana na mbinu zake nyingi za kiufundi.
Kocha huyo kwa sasa ndiye msingi wa pili wa Simba akiwa na , lakini anakosa nafasi ya kutosha kuthibitisha ufanisi wake kutokana na kulazimika kutekeleza kile anachopangiwa na Kocha Mkuu , wake Pierre Lechantre.
Makocha hao wameiweka Simba kileleni mwa ligi kwa sasa ikiwa na pointi 55 na Yanga inazo 47.
Chanzo: Mwananchi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here