Mwamuzi Simba, Yanga utata mtupu

0
16
 WAKATI siku 16 zikibakia kabla ya mechi ya Ligi Kuu baina ya Watani wa Jadi, Simba na Yanga kuchezwa, Refa aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo Emmanuel Mwandembwa huenda akabadilishwa kutokana na kuteuliwa kuchezesha mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 yanayofanyika Burundi kuanzia kesho.
Mwandembwa ni miongoni mwa waamuzi wa kati nane walioteuliwa kuchezesha mashindano hayo yanayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ambayo yatafanyika kuanzia Aprili 14 hadi 28 kwenye miji ya Ngozi, Muyinga na Gitega.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba na Yanga zimepangwa kukutana kwenye Uwanja wa Taifa, Aprili 29, siku moja baada ya kumalizika kwa mashindano hayo ambayo Mwandembwa aliyepangwa kuchezesha mchezo huo wa Watani wa Jadi atakuwa miongoni mwa waamuzi 16 walioteuliwa na CECAFA kuchezesha mashindano hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Chama alisema upo uwezekano mkubwa kwa Mwandembwa kubadilishwa iwapo hakutokuwa na uwezekano wa kuwepo nchini siku chache kabla ya mechi hiyo.
“Mabadiliko ya waamuzi hufanyika kwa mujibu wa kanuni na taratibu hivyo tunasubiria CECAFA watupe ratiba ya hayo mashindano kisha tutaangalia huyo mwamuzi mechi zake zitaishia siku gani na kisha kuona kama ataweza kuwahi hiyo mechi au la. Tukishapata taarifa kutoka CECAFA, nadhani tutalitolea ufafanuzi hilo siku chache zijazo.
Inawezekana ratiba yake kwenye hayo mashindano inaonyesha kwamba mechi atakazochezesha zitaisha siku nne kabla ya mechi ya Simba na Yanga ambazo zinamtosha kabisa kuwahi huo mchezo hivyo hatutombadilisha lakini pia inawezekana ratiba ikamtaka awepo hadi tarehe 28. Ikiwa hivyo hatutokuwa na namna zaidi ya kumbadilisha na kumpanga mwingine,” alisema Chama.
Gazeti hili lilipojaribu kuwasiliana na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Boniface Wambura,a alituma ujumbe kuwa yupo kwenye kikao.
Mbali na Mwandembwa, mwamuzi mwingine wa Tanzania Bara aliyeteuliwa kuchezesha mashindano hayo ni mshika kibendera Mohammed Mkono wakati kwa Zanzibar aliyeteuliwa ni Mbaraka Haule.
Wakati huohuo, timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imepangwa katika kundi B la mashindano hayo sambamba na timu za Sudan, Zanzibar na Uganda huku mechi zake zikipangwa kuchezwa kwenye mji wa Ngozi.
Kundi A la mashindano hayo ambalo mechi zake zitachezwa kwenye vituo vya Muyinga na Gitega linaundwa na timu za Burundi, Kenya, Ethiopia na Somalia.
Chanzo: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here