Kwa nini wanamichezo wanatoweka kwenye michezo ya kimataifa ulaya?

0
3


Waandalizi wa michezo ya Jumuiya ya madola inayofanyika nchini Australia wanasema kuwa wanariadha watano kutoka Afrika wametoweka.

Wanasema kuwa wanawatafuta wanamichezo hao ambao wanatoka Rwanda na Uganda.

Usakaji wa raia wanane wa Cameroon waliotoweka siku ya Jumatano bado unaendelea.

Waandalizi hao pia wanajaribu kuwatafuta wachezaji wawili wa mchezo wa squash kutoka Sierra Leoni.

Wanyanyuaji uzani watatu na mabondia wawili waliripotiwa kwa maafisa wa polisi wa Australia baada ya kutoweka tangu siku ya Jumanne, hatua iliozua hali ya wasiwasi kwamba walitoroka na hawana nia ya kurudi Cameroon.

‘Sababu za kiuchumi’

Katika michezo ya Olimpiki ya 2000 iliofanyika nchini Sidney wachezaji 80 walisalia nchini humo hata baada ya muda unaowaruhusu kukaa nchini humo kukamilika.

Waandalizi wa michezo hiyo wamewataka wanariadha kuheshimu sheria licha ya kwamba zaidi ya wanariadha 2000 waliishi nchini humo hata baada ya muda wao kukamilika.

Kabla ya michezo hiyo kuanza waziri wa maswala ya ndani nchini humo Peter Dutton, alionya kwamba wanariadha watachunguzwa kwa karibu ili kuhakikisha kwamba hawaendelei kusalia nchini humo hata baada ya michezo kukamilika.

Mwaka 2000, wanariadha saba wa Cameroon walitoweka katika michezo ya Olimpiki. Saba hao ni mabondia watano, muogeleaji na mchezaji mmoja wa soka. Waliamua kutorokea nchini humo kutokana na sababu za kiuchumi.

‘Theluthi mbili ya timu yapotea’

Katika ufunguzi wa sherehe za michezo ya jumuiya ya madola iliofanyika mjini Manchester 2002 Uingereza, haikuwa rahisi kuitambua timu ya Sierra Leone iliohudhuria michezo hiyo.

Kundi la wanamichezo wa Sierra Leone lilikuwa limebanwa katikati ya wachezaji wa Sychelles na Singapore.

Kelele zilizokuwa katika uwanja wa michezo hiyo zilitawala huku wachezaji hao wakikosa kutiliwa maanani na hata mtangazaji alisema kwamba wachezaji wa Sierra Leone wameingia na hii ni mara yao ya saba katika michezo hiyo.

Kulikuwa na wachezaji 30 wakionekana kuwa warefu na wembamba, walipunga mikono na kutabasamu na baadaye kamera ikawamwilika washiriki wa Singapore.

Lakini wakati wa sherehe za kufunga michezo hiyo wachezaji wa Sierra leone walionekana kupungua, lakini hakuna mtu aliyekuwa na shauku kuhusu idadi yao.

Wakati huo Sierra Leone haikushinda hata medali moja.

Siku hiyo kulikuwa na mvua iliokuwa ikinyesha, hivyo basi washindani wengine kutoka mataifa tofauti waliamua kusalia katika kijiji cha wanariadha ili kutonyeshewa.

Wanariadha wa Sierra leone walitarajiwa kuabiri ndege na kurudi nyumbani.

Lakini ni wakati thuluthi mbili ya wachezaji wa taifa hilo walipokosekana katika uwanja wa ndege ndipo sasa ukweli ukaanza kudhihirika.

Idadi kubwa ya wachezaji wa taifa hilo walikuwa wametoweka!

‘Kuzamia’

Sababu kuu ikiwa – wanamichezo kutoka mataifa masikini walitumia michezo hiyo katika taifa tajiri kutafuta uhifadhi kwa njia nyengine.

Mwezi Julai mwaka 2017, vijana sita wa Burundi waliokuwa wakishiriki katika mashindano ya roboti nchini Marekani waliripotiwa kutoweka, kwa mujibu wa polisi.

Wavulana wanne na wasichana wawili walio kati ya umri wa miaka 16 na 18 walipotea wakati wa mashindano hayo ya kwanza duniani yaliofanyika Washington DC.

Idara ya polisi mjini humo ilisema kuwa mara ya mwisho vijana hao kuonekana ilikuwa wakati wa makamilisho ya michezo hiyo.

Ripoti zinasema kuwa vijana wawili kati yao tayari walikuwa wamevuka mpaka na kuingia Canada lakini ripoti hiyo haikuthibitishwa na polisi.

Idara ya polisi mjini humo ilibandika picha za sura za vijana hao sita katika mtandao wao wa Twitter, wakiwataka raia kuwasiliana nao iwapo watakuwa na habari yoyote kuwahusu.

Waandalizi wa mashindano hayo waliwaeleza polisi baada ya msimamizi wa timu hiyo ya Burundi kushindwa kuwapata vijana hao.

‘Kutafuta hifadhi’
Mwaka 2012 wachezaji 17 kutoka timu ya soka ya Eritrea na muuguzi wao walitoweka nchini Uganda.

Ni wachezaji 12 pekee waliorejea kutoka ziara ya kununua bidhaa na kati ya hao, watano waliondoka baadaye wakisema walikuwa wanawatembelea marafiki zao, lakini hawakurejea.

Hii ilimaanisha ni wachezaji watano tu na maafisa wawili ambao walisalia kurejea Asmara.

Maafisa wa usalama walianzisha msako wa wachezaji hao waliotoweka walipokuwa mjini Kampala kushiriki mashindano ya CECAFA.

” Hatujui ndugu zetu wako wapi, ” alisema mkufunzi wa timu Teklit Negash

Tovuti ya chama cha Upinzani nchini Eritrea ilidai kuwa wachezaji hao walikuwa wanataka kuomba hifadhi ya kisiasa nchini Uganda, lakini madai hayo hayakuthibitishwa.

Katika michezo ya Olimpiki ya mjini London 2012, ujumbe wa watu wanne katika timu ya Olimpiki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ulitoweka jijini London.

Mshiriki wa mchezo wa Judo, na makocha wa timu za ndondi, riadha hawakuonekana wakati wa kumalizika kwa sherehe za kufunga michezo hiyo siku ya Jumapili.

Jamhuri ya Congo iliwakilishwa katika michezo ya London Olimpiki na wanamichezo wanne ambao hawakuweza kushinda medali yoyote.

Posted By Lebab

Source: Bbc

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here