Kisa Simba Chirwa arejea kwao Zambia

0
8

Jumatano wiki hii straika wa Yanga, Obrey Chirwa alienda kwao Zambia kutokana na matatizo ya kifamilia, sasa uongozi wa klabu hiyo umesema mchezaji huyo anarudi muda wowote kuanzia sasa kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba.

Chirwa hatacheza mechi ya leo ya Yanga dhidi ya Wolayta Dicha ya Ethiopia ya kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwani ana kadi mbili za njano, hivyo kwa mujibu wa kanuni hatocheza.

Chirwa alipata kadi hizo katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers ya Boswana.

Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alisema kuwa, Chirwa atarejea baada ya wiki moja ili kuwahi maandalizi ya mechi dhidi ya Simba itakayochezwa Aprili 29, mwaka huu.

“Chirwa aliondoka kwa ruhusa ya wiki moja kwenda nyumbani kwao kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia, hatutarajii akae sana huko kwa kuwa anatakiwa awahi kurudi kwa ajili ya maandalizi ya mechi yetu dhidi ya Simba,” alisema Ten. 

Chirwa ana mabao 12 kwenye Ligi Kuu Bara, na amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga kutokana na uhodari wake wa kuzifumania nyavu.

CHANZO: CHAMPION
Na: Agape Patrick
Email: agape@spoti.co.tz

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here