Huko Yanga ni moto, Lwandamina azuiwa

0
8
KAULI na mipango mikakati ndani ya mabosi wa Yanga ni kwanza, kuhakikisha Singida United hawatoki salama kesho Jumatano pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Lakini, mabosi hao wanatambua kuwa mchezo unaofuata baada ya Singida United ni wale Wahabesh, Welaytta Dicha ya Ethiopia, ambao nao watakutana na saprize moja matata sana kwenye mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga leo ilikuwa na mazoezi makali pale Uwanja wa Chuo Kikuu cha Polisi kujiweka sawa kuikabili Singida na kwamba, wanataka alama tatu tu ili kuendelea kuipa presha Simba ambayo jana ilichomoza na ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar pale Jamhuri, Morogoro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika amelieleza Mwanaspoti kuwa kama kuna mchezo unaofanyiwa mikakati ya maana basi ni ule wa marudiano dhidi ya Welaytta Dicha na ni lazima Yanga isonge mbele.
Alisema baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza, sasa wanakwenda kukamilisha kazi kule jijini Awassa, Ethiopia.
Tayari Nyika amesema wamekutana na benchi la ufundi chini ya George Lwandamina na kwamba, wanaamini sapraizi kwa Waethiopia hao ni ukamilifu wa kikosi chao kwenye mchezo huo wa Aprili 18.
Alisema kurejea kwa viungo Pappy Kabamba ‘Tshishimbi, Said Makapu, beki Kelvin Yondani na mshambuliaji Obrey Chirwa ni kama timu yao itakuwa mpya mbele ya Wahabeshi hao.
“Akili yetu iko kwa Singida ambao tunataka kuwamaliza kwanza kisha tuendelee na ishu zetu muhimu zaidi na baadaye tutaiangalia Simba, lakini zaidi ni kutinga hatua ya makundi,” alisema Nyika.
“Hawa Dicha tunawapelekea sapraizi ya maana tu kwani, hawaijui Yanga vizuri japo wanajaribu kutupeleleza, lakini hawawezi kabisa. Tumekutana na mwalimu na wachezaji na kila kitu kinakwenda vizuri.
“Yanga inatambua sasa ndio tunabeba sura ya nchi hivyo, tunachotaka ni ushindi tu hakuna zaidi ili tusonge mbele,” alisema.
DICHA WAITEGA YANGA CAF
Si unakumbuka kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa aliondolewa kwenye benchi katika mchezo dhidi ya Township Rollers ya Botswana, lakini katika orodha ya wachezaji wa Yanga na viongozi waliotakiwa kuwa nje dhidi ya Dicha, jina la nahodha huyo wa zamani halikuwepo kabisa.
Sasa kwa taarifa yako ni kwamba, mabosi wa Dicha walikuwa wamepiga kimya wakiomba Mungu Yanga wamweke Nsajigwa katika benchi ili wapeleke malalamiko Caf ambayo yangewafanya wana Jangwani hao kushushiwa rungu.
Caf, Shirikisho la Soka Afrika liliwazuia kucheza dhidi ya Dicha mastaa wanne wa Yanga ambao ni Tshishimbi, Makapu, Yondani na Chirwa, pia ilimzuia kocha msaidizi wa Yanga, Mzambia Noel Mwandila.
CAF kumzuia Mwandila walijichanganya kutokana na kocha aliyetakiwa kutumikia adhabu hiyo kuwa ni Nsajigwa, lakini Yanga wakashtukia mchezo.
Awali, Yanga walikaribia kumwambia Nsajigwa kukaa benchi, lakini Dicha walikuwa wakisubiri kosa hilo ili wamkatie rufaa kiulaini tu.
Mabosi wa Yanga akili zikafanya kazi fasta na kuwaweka jukwaani Nsajigwa na Mwandila huku Lwandamina akibaki na Juma Pondamali na Meneja wa timu, Hafidh Saleh.
Lwandamina azuiwa kusepa
Wachezaji wa Zesco ya Zambia juzi usiku walikuwa wakishangilia baada ya kuelezwa na mabosi wao kwamba, kocha wao wa zamani Lwandamina anarejea kufundisha tena kikosi hicho.
Baadhi ya wachezaji wakavujisha taarifa hizo kwa mashabiki na ghafla shangwe zikashika kasi huko mitaani, lakini amesikia hizo taarifa na amefunguka machache sana.
Lwandamina ameliambia Mwanaspoti jana kuwa, bado yuko Yanga na hajutii kuwepo kwake kwa kuwa uamuzi wake. Kibarua cha kocha wa Zesco kipo wazi baada ya aliyekuwepo kubwaga manyanga juzi baada ya matokeo mabovu ya timu yake.
Hata hivyo, Lwandamina amsema kule Zambia karibu nusu ya klabu zinataka huduma yake kutokana na rekodi zake bora, lakini hajafikiria kuiacha Yanga na akili yake ni kushinda mataji na kutamba kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nimesikia hizo taarifa (Anacheka) hakuna ukweli kuwa naondoka hapa kama ingekuwa hivyo ningefanya muda mrefu sana ila nimeamua kubaki Yanga kwa maamuzi yangu.
“Zambia kila wakati napokea ofa za timu kuhitaji nikafanye kazi na nina ofa nyingi sana, lakini ukweli bado nipo Yanga natumikia mkataba wangu,î alisema.
Chanzo: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here