Bocco, Okwi janga la Taifa

0
5


Dar es Salaam. Washambuliaji John Bocco, Emmanuel Okwi wameendelea kuvunja rekodi za ufungaji baada ya kuiongoza Simba kuichapa Prisons kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 58 na kuwaacha Yanga kwa pointi 11 katika mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Wakati Simba ikisaka ubingwa wake wa kwanza baada ya kusubiri kwa miaka mitano washambuliaji wake Okwi na Bocco wenyewe wameendelea kuvunja rekodi mbalimbali za ufungaji bora wa Ligi Kuu.
Okwi akiwa katika kiwango cha juu alifunga bao lake la 19 msimu huu kwa mkwaju wa penalti na kuifikia rekodi ya msimu wa 2011/12 iliyowekwa na Bocco akiwa  na Azam pamoja na ile Amiss Tambwe aliyoweka akiwa Simba msimu 2013/14.
Nahodha wa Simba, Bocco naye alifunga bao lake 14 msimu huu akiunganisha kwa kichwa krosi ya Erasto Nyoni iliyogonga mwamba na kurudi uwanjani katika dakika 35.
Idadi hiyo ya mabao 14, inamfanya Bocco kuivunja rekodi iliyowekwa na Michael Katende wa Kagera Sugar aliyefunga mabao 11 msimu wa 2007/08.
Pia, nahodha huyo amefikia rekodi ya msimu wa 2016/17 iliyowekwa washambuliaji Simon Msuva (Yanga)  na Abdulraham Mussa ambao walitwaa tuzo ya ufungaji bora kwa kufunga mabao 14 kila mmoja.
Timu zote mbili zimeanzisha vikosi ambavyo vina mabadiliko zikianzisha baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa hawapati nafasi mara kwa mara.
Simba imemuanzisha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ anayechukua nafasi ya Nicholas Gyan aliyepo benchi wakati Prisons imewaanzisha Leons Mutalemwa na Cleophace Mukandala wanaochukua nafasi za Laurian Mpalile na Michael Ismail ambao wamekosekana kwenye mechi ya leo
Simba ilianza mchezo wa leo taratibu huku Prisons ikicheza kwa kulinda zaidi jambo lililofanya mchezo huo kuwa mgumu kwa timu zote.
Dakika 35, Nyoni alipiga krosi hiyo baada ya kufanya kazi nzuri ya kumuhadaa beki Benjamin Asukile wa Prisons na kupiga krosi hiyo ambayo ilimshinda kipa Aron Kalambo na kugonga mwamba kabla ya kumkuta Bocco.
Kiujumla Simba wametawala kipindi cha kwanza wakitengeneza takribani nafasi tano za mabao lakini walinzi wa Prisons wamekuwa imara kuokoa hatari hizo.
Prisons wameonekana kucheza soka la kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza lakini hata hivyo yameonekana hayana madhara kwenye lango la Simba.
Dakika 80, Okwi alitoa pasi kwa Bocco wakati anataka kupiga shuti aliangushwa na beki wa Prisons na mwamuzi Shomari Lawi akatoa penalti hiyo.
Okwi akifanya makosa alizamisha wavuni mpira huo na kuwahakikishia Simba pointi tatu muhimu.
Katika michezo mingine Ndanda ikiwa nyumbani ilikubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Ruvu Shooting, wakati Kagera Sugar waliamka kutoka nyuma na kuwachapa ndugu zao wa Mtibwa Sugar kwa bao 2-1.
Vikosi
Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Yusuph Mlipili, Murushid Juuko, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya, Jonas Mkude, John Bocco, Emmanuel Okwi, Asante Kwasi
Prisons: Aron Kalambo, Benjamin Asukile, Leons Mutalemwa, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya, Cleophace Mukandala, Mohammed Rashid, Freddy Chudu, Eliuter Mpepo
Msimamo Ligi Kuu  Bara 2017/2018
                          P W     D       L        F       A       PTS
1. Simba        24         17     7       0       57     12     58
2. Yanga         22        13     8       1       39     12     47
3. Azam          25        12     10     3       24     12     46
4. Prisons       25        9       11     5       23     18     38
5. Singida                25        9       10     6       22     23     37
6. Mtibwa    24          8       9       7       20     18     33
7. Ruvu           25        8       8       9       25     30     32
8. Lipuli          25        7       10     8       11     19     31
9. Stand          25       7       7       11     19     30     28
10.Kagera      25        5       11     9       17     25     27
11.Mwadui      25     5       11     9       27     34     26
12.Mbeya       24       5       11     8       21     28     26
13.Ndanda     25       4       11     10     17     26     23
14.Mbao        25       5       9       11      23    33     24
15.Majimaji    25      3       11     11     23     35     20
16.Njombe     25       3       10     12     14     33     19
 Chanzo: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here