Yaani Msuva bado kidogo tu

0
4
NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, ameingia anga za Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa na kama ataamua kukaza kidogo tu, atajiweka katika nafasi ya kuweka rekodi kwa wachezaji wa Kitanzania katika michuano ya CAF.
Ndio, Msuva anayeichezea Difaa Al Jadida ya Morocco iliyoingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika anashikilia nafasi ya pili ya orodha ya vinara wa mabao katika michuano ya msimu huu akiwa na mabao manne.
Mabao hayo ni pungufu kwa mawili yaliyofungwa na Samatta katika msimu wake wa kwanza wa michuano ya CAF akiwa na TP Mazembe alipofunga mabao sita katika mechi nane za Kombe la Shirikisho mwaka 2013 na kuwa mmoja wa vinara wa msimu huo.
Ngassa naye alimaliza akiwa Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014 akifunga pia mabao sita katika mechi nne, kabla ya mwaka uliofuata Samatta kuibuka kidedea na mabao yake saba katika mechi 14 wakati Mazembe ikibeba ubingwa wa Afrika.
Kwa mabao manne aliyonayo Msuva ana nafasi kubwa ya kuwafunika Samatta na Ngassa kama ataendelea kutupia mfululizo kama alivyofanya katika mechi nne zilizopita za timu yake, ingawa upinzani unaweza kuanzia ndani ya Al Jajida.
Kinara wa mabao kwa sasa wa Ligi ya Mabingwa ni Hamid Ahaddad wa Al Jadida mwenye mabao sita sawa na Hichem Nekkaache wa MC Alger ya Algeria.
Msuva alifunga Hat Trick katika mechi yao ya raundi ya awali dhidi ya Sport Bissau Benfica ya Guinea Bissau kabla ya kuongeza jingine raundi ya kwanza dhidi ya AS Vita ya DR Congo na kusaidia kuivusha timu yake iliyolazimisha sare ya 2-2 ugenini.
Msuva alinukuliwa akisema kiu yake ni kuendelea kufunga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here